Tume ya Huduma za Umma imewaonya Wakenya kuwa makini dhidi ya matangazo ya kupotosha yanayohusu nafasi za ajira serikalini kwenye mitandao ya kijamii.
Tahadhari hii inafuatia kisa ambapo machapisho ya matangazo ya nafasi za ajira , yamesambazwa kwenye mitandao ya kijamii yakionesha uwapo wa nafasi za kazi.
Inaarifiwa kuwa matangazo hayo yana hitaji la mtu anayetafuta kazi kutakiwa kutuma pesa kwa nambari za simu hali ambayo inakiuka utaratibu wa uajiri serikalini.
Majuma mawili yaliyopita, kisa sawa na hiki kilishuhudiwa mitandaoni ambapo matangazo ya nafasi za ajira kwenye idara ya usajili wa watu, yalitangazwa na baadaye kutajwa kuwa potovu.
Wakenya wameshauriwa kushirikiana na maafisa wa usalama katika kutoa taarifa muhimu kuhusu walaghai wanaotumia mitandao ya kijamii katika kuwaibia wananchi.