Rais awaonya watakaovuruga marudio ya uchaguzi wa Urais
Na: Beatrice Maganga
Rais Uhuru Kenyatta leo hii ameongoza maadhimisho ya sherehe za Mashujaa huku akiwoanya vikali watakaozua vurugu wakati wa marudio ya uchaguzi wa urais, Alhamisi wiki ijayo. Rais aidha amewaonya wanaohujumu utendakazi wa Tume ya Uchaguzi, IEBC kwa lengo la kutatiza maandalizi ya uchaguzi huo huku akiwarai wananchi kumpa fursa nyingine tena ya kuliongoza taifa ili wanufaike zaidi kupitia miradi ya maendeleo kukiwamo elimu bila malipo katika shule za sekondari za umma kuanzia mwezi Januari mwaka ujao. Wakati uo huo, ametangaza mpango wa kubuniwa kwa Baraza la Mashujaa kwa lengo la kutambua juhudi za watu mbalimbali nchini.
Wakati wa kuhutubu, Rais Uhuru Kenyatta akatoa onyo kali kwa wanaoelenga kuzua vurugu wakati wa marudio ya kura ya urais akisema watakabiliwa vilivyo. Rais amesema vikosi vya usalama vimetumwa kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kudumisha usalama na kuwawezesha watakaojitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura.
Rais aidha amewashauri wananchi kujiepusha na viongozi anaowataja kuwa wachochezi huku akisema wanaopania kuandamana, wana uhuru wa kufanya hivyo japo hawatasazwa iwapo watatatiza amani na utendakazi wa IEBC.
Sherehe za leo zimehudhuriwa na wananchi na viongozi wa matabaka mbalimbali. Jaji Mkuu, David Maraga, naibu wake, Philomena Mwilu, Mwanasheria Mkuu wa serikali Profesa Githu Muigai, Spika wa Bunge la Kitaifa, Justine Muturi mwenzake wa Seneti Kenneth Lusaka, mabalozi wa mataifa mbalimbali ni miongoni mwa waliohudhuria wakiwamo mawaziri na mabalozi.
Awali, siku ya Mashujaa ilitambuliwa kuwa Kenyatta Day, kwa ajili ya kumbukumbu za Hayati Mzee Jomo Kenyatta pamoja na mashujaa wengine wakiwamo Paul Ngei, Kung'u Karumba, Fred Kubai, Bildad Kaggia na Achieng Oneko, kabla ya kubadilishwa chini ya katiba mpya mwaka 2010 kuwa Siku ya Mashujaa.
.........................?