Na Beatrice Maganga/ Mike Nyagowoka
Huku Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne, KCSE ukiingia siku ya pili leo, maafisa wa ngazi za juu katika sekta ya elimu wameendelea na misururu ya ziara kukagua mchakato wa kufanywa kwa mtihani huo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Dkt. Belio Kipsang amekagua shughuli hiyo kwenye eneo la Isinya, Kaunti ya Kajiado. Waziri wa Elimu Fred Matiang'i kwa upande wake amefika katika Shule ya Wasichana ya Karimi.
Maafisa hao wamesema wataendelea kukagua shughuli hiyo hadi mtihani huo utakapokamilika baadaye mwezi huu. Dkt. Kipsang amesema maafisa wa Wizara ya Elimu wanashirikiana na wale wa Wizara ya Masuala ya Ndani ya Nchi ili kuhakikisha kuwa hakuna kisa chochote cha udanganyifu kinachoshudiwa mwaka huu jinsi ilivyokuwa miaka ya awali.
Hayo yakijiri, afisa mmoja aliyekuwa akisimamia mtihani wa KCSE kwenye Kaunti ya Mombasa amefikishwa mahakamani leo hii kwa madai ya kujaribu kufanikisha udanyanyifu. Afisa huyo, Dennis Juma Were aliyekuwa akisimamia mtihani katika Shule ya Mikindani Complex anakabiliwa na tuhuma za kufungua karatasi za Somo la Kemia.
Hata hivyo amekana mashtaka dhidi yake mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Mombasa, Teresia Mwatheka na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi laki tano. Kesi dhidi yake itatajwa tena Disemba kumi na tatu.
Kwingineko, polisi kwenye Kaunti ya Murang'a wanaendeleza uchunguzi kufuatia kisa cha kutoweka kwa mwalimu mmoja mkuu. Solomon Mwangi aliripotiwa kutoweka tangu Jumapili na hajaonekana katika kituo cha kuzihifadhi karatasi za mtihani, ambapo alitarajiwa kuzipeleka shuleni mwake.