Namwamba atafaulu kutatua shida zinazokumba wanamichezo?

By - Jan 1st 1970

Ni nadra sana kuzipata habari njema za michezo, hasa soka, kutoka nchini Kenya. Hii ikichangiwa pakubwa na hatua ya aliyekuwa Waziri wa Michezo Dr. Amina Mohamed kuvunjilia mbali lililokuwa shirikisho la soka nchini FKF.

Kuvujiliwa mbali kwa FKF, kuliandamwa na kufungiwa nje kwa soka la Kenya na shirikisho la soka duniani, FIFA. Kwa maana hii ni kuwa mama Amina aliachia ‘uongozi’ wa soka mikononi mwa kamati simamizi/kamati andalizi na kila aina ya kamati. Matokeo yake je? Marufuku yakawa kwa miezi tisa!

Marufuku bado yakiwa, timu za taifa za Kenya, Harambee Stars na Starlets, hazingeweza kushiriki mechi za kimataifa. Vivyo hivyo, vilabu husika kwa maana ya kuyatwaa mataji ya ligi, mathalan mabingwa wa ligi ya soka nchini Tusker, hawakuweza kushiriki mechi za kimataifa kwa maana ya klabu bingwa barani Afrika.

Marefari wetu watajika wa viwango vya FIFA wakiongozwa na mhadhiri Dr. Peter Waweru, wangepata fursa ya kuenda Doha nchini Qatar, kwa minajili ya kuwa waamuzi kwenye baadhi ya mechi za kombe la dunia.

Yote haya yalitokana na mshikemshike wa utawala wa soka ambao ulivigonganisha vichwa viwili: Cha Dr. Amina na aliyekuwa rais wa wa FKF Nick Mwendwa. Kamati iliyochukua uongozi wa soka nchini iliishia kuwa vituko, maajabu na zigo-zigo la kuchafua hewa na kuiachia nchi ikiwa katika njia-panda. Mashabiki wakapiga kelele hadi sauti zikawapwelea.

Rais aliyeondoka mamlakani Uhuru Kenyatta, na aliyekuwa Waziri wa Michezo Dr. Amina Mohammed wakaiacha nchi ikiwa katika hamkani. Soka likakufa fo! Alipohojiwa na Radio Maisha, kwenye makala ya DANADANA VIWANJANI, Barry Otieno alisema kuwa kipindi hiki cha marufuku, wamepoteza zaidi ya Sh700 milioni. Yaani kukawa KUBAYA!

Punde baada ya rais Dr. William Ruto kutawazwa kuwa rais wa awamu ya tano, akamteua Dr. Ababu Namwamba, kuwa waziri wa michezo. Punde baada ya Ababu kuingia mamlakani baada ya kupigwa msasa na kamati ya bunge, aliahidi kuwa kibarua chake kikubwa ni KUIREJESHA soka kwenye ramani ya Afrika na dunia.

Na kama ngariba aliyekiona kisu, Dr. Ababu amepiga kazi kweli! Chanda chema huvishwa pete! Cha jasho hakikosi utamu.

Waziri wa Michezo, Dr. Ababu Namwamba, mara tu baada ya kula kiapo, amekuwa na vikao na wenyeviti/maafisa wakuu wa vilabu, kamati kuu ya usimamizi wa FKF na wadau wengineo. Kwa bahati nzuri, vikao hivi vimezalisha matokeo yenye faida. Natija.

Usimamizi wa FKF (Baraza Kuu), chini ya uangalizi wa Naibu Rais, Dr. Doris Petra na Afisa Mkuu Barry Otieno, wamerejeshwa afisini katika makao makuu yaliyoko Kandanda House. “Rais” wa FKF Nick Mwendwa ameambiwa kujiondoa kwa muda huku akisubiri maamuzi kuhusu kesi ya ufisadi inayomkabili.

Kwa kweli, ahadi ni deni, na dawa ya deni ni kulipa. Waziri wa michezo Dr Namwamba alipokuwa akihojiwa na kamati maalum ya bunge, aliahidi kuwa simu yake ya kwanza ingekuwa kwa rais wa shirikisho la duniani, FIFA, Gianni Infantino.

Wiki hii, waziri Namwamba alikuwa Qatar kwenye fainali za kombe la dunia, alikofanikiwa kukutana na Infantino. Habari njema ni kuwa FIFA imeiondolea Kenya marufuku. Ingawa hivyo, mashirikisho mengine yangali kukumbwa na misukosuko.

Imebaki sasa tuone vile waziri Dr Namwamba atakabiliana na changamoto ambazo bado zajitokeza. Mathalani, kwa sasa, wanaraga wanatembeza mabakuli ya ombaomba. Lakini tuna matumaini, kwa sasa wacha kazi iendelee!

akaulen@standardmedia.co.ke

Share this story
.
RECOMMENDED NEWS