Wanafunzi,wasomaji,wasikilizaji na watazamaji,wanaamini sana vyombo vya habari Picha: Hisani

Zama hizo za mababu, tulikuwa twaambiwa kuwa ukisikika mngurumo wa ndovu, basi ni bayana kuwa umefika msimu wa mvua! Kauli hiyo hapo juu naitumia kwenye makala ya leo kuashiria wazi kuwa ndovu, kwa maana ya wasikilizaji wa redio, watazamaji wa runinga na wasomaji wa magazeti, bila kuwasahau wanafunzi, walimu na wadau wote wa lugha (ndio ndovu) na wamekwisha kunguruma!

Hivi najaribu kusema nini?

Wiki jana nimefanikiwa kupokea barua-meme kutoka kwa msikilizaji wangu na msomaji wa makala haya Bw. Khamis Kassim, ambaye ni mwalimu na tena mpenzi-ashiki wa lugha hii ashirafu ya Kiswahili. Kwenye barua-meme yake alikuwa na manung’uniko mengi tu. Akilalama jinsi ambavyo siye wanahabari, baadhi yetu, tunavyokiboronga na kukivyoga Kiswahili.

Hebu ninikuu aya mbili kwenye barua-meme yake: “Iweje sisi walimu wa Kiswahili tuwe twakichangamkia Kiswahili, twafanya utafiti na kufunza Kiswahili sanifu, lakini wanahabari wanakipotosha na hapo wanafunzi kutuhoji sisi walimu kwa kuwa wanaamini sana wanahabari.”

Hapo juu ndugu yangu imebainika kuwa wanafunzi, wasomaji, wasikilizaji na watazamaji, wanaamini sana vyombo vya habari. Na kwa hakika hili hujitokeza sana kila Jumamosi niwapo hewani radio maisha kwenye kipindi cha NURU YA LUGHA.

Hata hivyo, baada ya kupokea barua-meme hiyo, nilisemezana na msomaji wangu huyu ili kupata mfano wa hicho kinachomkosesha mno usingizi na kuutia majonzi mtima wake. Alinijibu hivi, “Neno tetesi nyie wanahabari mwalipotosha ni kama nini. Kama hilo halitoshi, ni kama nyie wanahabari hamjui kuhesabu tu idadi. Mwatupa dhiki jamani. Hebu Hassan mwana wa Ali liangazie hili...”

Ni kweli kuwa wanahabari hatujui maana ya neno tetesi ilhali makamusi tunayo matopa kwa matopa? Hivi ni ukweli kuwa hatujui tarakimu jamani? Inasikitisha moyo na kuunguza maini. Ni kama tunawakeketa mashabiki wetu kwa msumeno moto! Neno ‘tetesi’ linarejelea minong’ono, madai na muktadha kama huo. Mathalan, tetesi zaarifu kuwa...yaani minonng’ono na madai. Yaani hatuna yakini. Hatuna hakika. Lakini leo hii siye wanahabari, baadhi yetu, tumesikika tukisema hewani kuwa mshukiwa katoa tetesi zake mahakamani, tukirejelea utetezi. Ewe!

Hili la idadi nalo ndio tusiseme. Nakubaliana na ndugu yangu Bw. Khamisi. Mia fil-mia tena. Ni mara ngapi tumesikika tukisema watu watisa badala ya tisa, mabao mbili badala ya mawili, watu kumi na mbili badala ya kumi na wawili. Wanafunzi wasaba badala ya saba. Magoli tatu badala ya matatu. Idadi ni ndefu. Twajijua jamani.

Kama anavyosema mwalimu na mwandishi-mtajika Wallah bin Wallah kwenye NURU YA LUGHA kila Jumamosi, ni kuwa matatizo hayo ya kutojua kuambisha vyema idadi, iwe ya watu, mifugo, mabao, viti, vitu na vinginevyo, inachangiwa pakubwa na baadhi yetu wanahabari kutozimanya, kuzitwalii na kuzidhibiti vyema ngeli za Kiswahili. Twaambiwa kuwa hakuna mjuzi wa wajuzi ela Mwenyezi Mungu pekee. Hivyo basi naomba kwa unyenyekevu, napiga magosti hasa, kwa wanahabari wenzangu sio tu kuwa makini lakini tuwe tayari kukosoana na kunyooshana tunapoteleza kuliko kunyamaa na kuwaachia wakosoaji na wahakiki kuiponda tasnia yetu hii tamu kama haluwa ya uanahabri, au siyo?

Hassan mwana wa Ali ni nahodha wa NURU YA LUGHA na Mhariri wa Michezo (Radio Maisha)

Barua-meme:alikauleni@gmail.com, akaulen2@standardmedia.co.ke FB: Ali Kauleni Hassan, Hassan mwana wa Ali

Twitter: @alikauleni