Mbunge wa Kapsaret, Oscur Sudi atalazimika kukaa korokoroni kwa siku nyingine saba ili kuwapa polisi muda wa kufanya uchunguzi kuhusu matamshi ya uchochezi yanayomkabili. Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Nakuru, Joseph Kalu ametoa uamuzi huo akisema Sudi atalazimika kukaa huko hadi atakapotoa uamuzi wa iwapo atamwachilia kwa dhamana ama la.
Tayari mbunge huyo alikuwa amekaa katika seli za Kituo cha Polisi cha Nakuru kwa siku mbili akisubiri uamuzi wa leo wa mahakama wa iwapo ingemwachilia kwa dhamana ama la. Baadhi ya viongozi wa Tangatanga walioandamana na Sudi wakati wa kutolewa kwa uamuzi, wamesema wanaheshimu sheria na kwamba watazingatia maagizo ya mahakama hadi kesi dhidi ya mbunge huyo itakapokamilika. Seneta wa Nakuru, Susan Kihika na Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri ni miongoni mwao.
Awali mmoja wa mawakili wake alielezea matumaini kwamba Sudi angeachiliwa kwa dhamana akisema makosa anayodaiwa kuhusika hayatoshi kuendelea kumzuilia. Anakabiliwa na mashtaka matano ambayo ni kutoa matamshi ya uchochezi, kumpiga afisa wa polisi, kukiuka maadili, kukataa kukamatwa vilevile kumiliki silaha kinyume na sheria.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Daniel Karuri ulipinga kuachiliwa kwake kwa dhamana ukisema huenda akawatishia mashahidi ikizingatiwa ushawishi wake katika jamii.
Ikumbukwe wikendi iliyopita, wafuasi wa Sudi walikesha nyumbani kwake kuwazuilia polisi wasimkamate kwa tuhuma za kumdhalilisha Rais Uhuru Kenyatta na familiaa yake. Hata hivyo hatimaye mbunge huyo alijiwasilisha katika Kituo cha Kapsaret kwenye Kaunti ya Uasin Gishu kabla ya kusafirishwa hadi Nakuru ambapo aliwasilishwa mahakamani.
READ MORE
Former magistrate Orenge sacked for gross misconduct
Fact-check: How many boda bodas or 'kisiagi's' can you buy with Sudi's Sh145m donation?