Shirika la Chakula Duniani (WFP) limesema kwamba kupunguzwa kwa ufadhili kutazidisha mgogoro wa njaa unaozidi kuongezeka kote duniani.
Shirika hilo limeonya kwamba zaidi ya watu milioni 300 watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka ujao.
Ripoti ya WFP ya Global Outlook ya mwaka wa 2026 inaashiria kwamba uhaba wa chakula unatarajiwa kuongezeka.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema inakadiriwa kuwa watu milioni 318 watakabiliwa na ukosefu wa uhakika wa chakula mwaka ujao, idadi ambayo ni zaidi ya mara mbili ya mwaka wa 2019.
Kati ya hawa, karibu milioni 41 wanakadiriwa kuwa katika awamu ya ‘dharura’ au mbaya zaidi, ambayo ni sawa na uainishaji wa usalama wa chakula IPC 4, Integrated Food Security Phase Classification (IPC) Phase 4 au zaidi katika mfumo wa ufuatiliaji wa njaa unaokubalika duniani.
WFP inatarajia kuweza kulisha takriban watu milioni 110 ifikapo mwaka 2026, na kuacha idadi kubwa ya watu duniani wakihitaji msaada wa chakula bila msaada wake.
Mintarafu ya hayo shirika hilo limesema linakadiria kuwa hitaji lake la uendeshaji wa shughuli za utoaji wa misaada litafikia dola bilioni 13 mwaka 2026, huku fedha nyingi zikitumika katika kukabiliana na majanga na gharama zingine, ikiwa ni pamoja na kujenga ustahimilivu na kushughulikia sababu kuu.
Utabiri wa sasa unaonesha kwamba WFP inaweza kupokea karibu nusu ya kiasi hicho pekee.
"Dunia inakabiliwa na njaa inayotokea kwa wakati mmoja, huko Gaza na sehemu za Sudan. Hili halikubaliki kabisa katika karne ya 21," Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain amesema katika taarifa.
"Njaa inazidi kuimarika. Tunajua suluhisho za mapema na zenye ufanisi huokoa maisha, lakini tunahitaji sana usaidizi zaidi," Cindy McCain ameongeza.
Katika Jiji la Gaza na maeneo ya jirani, IPC ilitangaza njaa mwezi wa Agosti, miezi kadhaa baada ya jeshi la Israeli kuweka kizuizi kamili cha miezi kadhaa dhidi ya Gaza. Mgogoro wa njaa katika eneo lote la Palestina bado ni mbaya huku Israeli ikiendelea kuweka vikwazo kwenye usambazaji wa chakula, mafuta, maji na dawa.
Hali ya njaa ilithibitishwa katika maeneo ya el-Fasher na Kadugli ya Sudan mapema mwezi huu, pamoja na maeneo mengine 20 huko Darfur na Kordofan – maeneo ya mapigano kati ya Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vya kijeshi RFS na jeshi la Sudan – yaliyo hatarini kukumbwa na njaa.
Afghanistan, Yemen, Syria, Sudan Kusini, eneo la Sahel la Afrika Mashariki, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Haiti na Nigeria ni baadhi ya maeneo mengine yanayotia wasiwasi.
Migogoro inasalia kuwa kichocheo kikuu cha njaa duniani kote, huku zaidi ya theluthi mbili ya ukosefu wa uhakika wa chakula ukisababishwa na migogoro inayosababishwa na mapigano.
Kulingana na WFP, mabadiliko ya hali ya hewa, kukosekana kwa utulivu wa kiuchumi, na mfumuko wa bei ya chakula na nishati vinazidisha hali hiyo.