Mwanaharakati Bob Njagi amedai kuwa kutekwa nyara kwake pamoja na mwenzake Nicholas Oyoo nchini Uganda kulipangwa na serikali ya Kenya. Njagi ameeleza kwamba walikamatwa na kikosi cha kijeshi kinachofanya kazi chini ya uongozi wa Jenerali Muhoozi Kainerugaba wa Jeshi la Ulinzi la Uganda UPDF, huku akiongeza kuwa zaidi ya watu 150 wanazuiliwa bila kufikishwa mahakamani kwa sababu za kisiasa.
Akiwahutubia wanahabari, Njagi alisema kuna ushirikiano kati ya Kenya, Tanzania na Uganda katika kuwakandamiza wakosoaji wa tawala zao, jambo ambalo limeongeza hofu miongoni mwa wanaharakati na viongozi wa upinzani.
Wawili hao walikuwa wametoweka kwa siku 38, na waliporejea walidai kuwa waliteswa na kunyimwa chakula wakiwa katika kambi ya kijeshi ya Kasenyi, Entebbe. Njagi alisema hali hiyo ilikuwa ni sehemu ya mbinu za kikatili zinazotumika ili kunyamazisha wagombea wa upinzani na wanaharakati wanaotoa maoni tofauti na serikali ya Uganda.
Walikamatwa walipokuwa wakishiriki katika kampeni za mgombea urais wa National Unity Platform-NUP, Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, ambaye amemshtumu Rais Yoweri Kaguta Museveni kwa kutumia utekaji nyara kuwanyamazisha wakosoaji wake. Hata hivyo, Njagi amekana kushirikiana na Bobi Wine katika mipango yoyote ya kuvuruga amani nchini humo, na kufafanua kuwa lengo lake ni kudai haki za kibinadamu na uwajibikaji wa serikali.
Rais Museveni tayari amekiri kuwa wanaharakati hao walikamatwa na asasi za usalama, akiwashutumu kwa kupanga ghasia kwa kushirikiana na Bobi Wine.
Njagi amesisitiza kuwa madai haya si sahihi na hayana msingi, huku akionyesha hofu yake juu ya visa vingi vya utekaji nyara vinavyofanyika nchini Uganda chini ya uangalizi wa Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Mwanaharakati huyo ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia hali ya usalama na haki za binadamu nchini Uganda na kuhakikisha wanaharakati wanapata huru bila masharti.