Kenya imeungana na mataifa mengine duniani kuadhiminisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka wa 2022 ni Uandishi wa Habari katika mazingira tata ya kidijitali.

Siku hii huadhimishwa kila tarehe 3 ya mwezi Machi lengo kuu likiwa kuzikumbusha serikali kuhusu umuhimu wa kuheshimu, kudumisha na kuunga mkono uhuru wa vyombo hivyo ikizingatiwa mchango wa vyombo hivyo kwa jamii.

Aidha, wanahabari waliofariki dunia wakiwa kazini pamoja na waliokamatwa au kuteswa wakitekeleza majukumu yao vilevile husherehekew a wakati wa maadhimisho haya.

David Omwoyo ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Vyombo vya Habari nchini Kenya MCK, ameendelea kukariri haja ya waajiri kuboresha mazingira ya kikazi kwa wanahabari pamoja na kuongeza mishahara kwa wale wanaopata malipo duni.

Akizungumza na Radio Maisha, Omwoyo aidha amekashifu visa vya wanahabari kuvamiwa wanapokuwa kazini, akitoa wito kwa washikadau mbalimbali kulinda haki za wanahabari.

Maadhimisho haya yanajiri wakati wanahabari nchini  Kenya wameendelea kukandamizwa, japo visa hivyo vimepungua kwa asilimia kubwa.

Cha hivi punde ni kile cha wanahabari 2 wa The Standard na mwenzake wa The Star kuvamiwa na wahuni waliodaiwa kuwa walinzi katika Jumba la Orange House kutokana na taarifa walizochapisha kuhusu uteuzi wa chama cha ODM.