Na Carren Omae
Licha ya Waziri wa Elimu, Fred Matiangi kutoa onyo kali dhidi ya watakaoshiriki udanganyifu katika mitihani ya kitaifa, mwalimu mkuu wa shule moja, afisa wa polisi wa utawala na afisa wa usimamizi wa mtihani wa KCSE, wamekamatwa kwa tuhuma zinazohusu uhalifu huo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Gatuanja eneo la Nyeri na maafisa hao wamekamatwa baada ya kushukiwa kushiriki wizi wa Somo la Kemia huku Mkuu wa Polisi, Larry Kieng akisema watafikishwa mahakamani kesho.
Mapema leo, Waziri Matiang'i amesema serikali haitawavumilia maafisa wasiowajibika katika kuzuia udanganyifu katika mitihani. Ameongeza kuwa serikali ilitenga rasilimali za kutosha kuwafunza maafisa watakaosimamia mitihani kote nchini mwaka huu, huku akisema visa sawa na vilivyoshuhudiwa mwaka jana havitaripotiwa.
Alikuwa akizungumza kwenye eneo la Murang'a alipofika alfajiri kushuhudia shughuli ya kuanza kwa mtihani huo.
Hayo yakijiri, Baraza la Mitihani KNEC limedhibitisha kupokea taarifa kwamba kuna baadhi ya watu wanaodai kuuza karatasi za mitihani. Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Baraza hilo limesema hakuna mtihani wowote ilioibwa na karatasi hizo ni bandia. Mwenyekiti wa KNEC George Magoha amesema wamehakikisha kwamba karatasi hizo hazifanani na zile za mitihani ya KCSE iliyoanza leo hii.
Magoha amesisitiza kwamba ilivyokuwa wiki jana wakati wa mitihani ya darasa la nane KCPE, usalama utaimarishwa hata mara dufu. Amewaonya wananchi kuwa waangalifu na kutozinunua karatasi zinazouzwa.
Takribani watahiniwa elfu 577, 253 wanafanya mtihani huo mwaka huu wakilinganishwa na elfu 522,870 mwaka jana.