Na, Sophia Chinyezi

Benki za humu nchini zimepoteza katika jitihada zao za kuzuia kudhibitiwa kwa viwango vya riba vinavyotozwa wanaochukua mikopo, baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusaini kuwa sheria Mswada wa Marekebisho wa Benki wa mwaka 2015. Hatua hiyo inazizuia benki kuongeza riba zinazotozwa mikopo kuwa zaidi ya asilimia nne ya riba iliyoratibiwa na Benki Kuu. Huku Benki Kuu ikiwa katika asilimia 10.5, benki sasa haziwezi kutoza riba ya zaidi ya asilimia 14.5 kwa mikopo.

Rais Kenyatta amesema licha ya juhudi za kupunguza riba kupitia mazungumzo, benki zimekuwa zikikosa kutekeleza maafikiano, badala yake kuendelea kuongeza viwango vya riba. Rais amesema ameafikia uamuzi wa kusaini mswada huo kuwa sheria baada ya mashauriano ya kina na washikadau mbalimbali wakiwamo wale wa benki. Aidha kupitia mashauriano hayo, Rais anasema alibaini kwamba Wakenya wamekuwa wakifadhaishwa na suala la benki kutojali maslahi yao kwa kuongeza viwango vya riba.

Hayo yakijiri, Muungano wa Benki Nchini KBA umesema utaheshimu mswada ambao umesainiwa kuwa sheria na Rais Kenyatta kwa lengo la kudhibiti viwango vya riba. Muungano huo hata hivyo umesema huenda watakaokuwa na nia ya kuchukua mikopo ya viwango vikubwa vya fedha wakaathirika. Aidha umelalama hakuna ushahidi unaoonesha kwamba hatua hiyo itawasaidia Wakenya wote wanaochukua mikopo kutoka katika benki.?