Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi, KEMFRI imekuwa ya hivi punde kuipongeza hatua ya Rais Uhuru Kenyatta kupiga marufuku utumiaji wa chupa za plastiki katika mbuga za kitaifa, misitu na kwenye fuo za bahari kuanzia tarehe tano mwezi Juni mwaka ujao.

Meneja wa tasisi hiyo, Erick Ochieng amesema hatua hiyo itakabili athari kwa wanyama wa baharini ambayo imekuwa ikisababishwa na utupaji ovyo wa taka za plastiki.

Amesema kwamba tayari matunda ya serikali kupiga marufuku ya utumiaji wa mifuko ya karatasi za plastiki mwaka jana, yameanza kuonekana kwani sekta ya uvuvi imeanza kuimarika upya.

Ameeleza imani ya sekta hiyo kuimarika hata na zaidi endapo marufuku hayo yatatekelezwa kikamilifu.

Kauli ya KEMFRI inajiri siku moja tu baada ya Wizara ya Utalii kusema marufuku hayo yataimarisha zaidi usafi wa mazingira kwenye maeneo hayo ambayo ni kivutio cha watalii wengi wanaozuru humu nchini.

Rais Uhuru alitangaza marufuku hayo wakati wa hotuba yake katika kongamao la mazingira jijini Vancouver, Canada.