Seneta wa Nandi Samson Cherargei amemtaka Gavana Stephen Sang kujiuzulu kufuatia tuhuma za ufisadi la sivyo atawaongoza wakazi wa kaunti hiyo kumtimua afisini.

Akiwahutubia wanahabari nje ya majengo ya bunge, Seneta Cherargei amesema zaidi ya shilingi bilioni 2.3 haziwezi kuwajibikia kwenye serikali ya Gavana Sang. Amemsihi Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi, DCI kumchunguza gavana Sang kufuatia utumizi mbaya wa ofisi.

Aidha Cherargei ameibua madai kwamba Sangi alitumia shilingi bilioni 2.6  kwa safari za ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Wilson hadi Maasai Mara ili kuvinjari.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya Gavana Sang kuwasimamisha kazi kwa muda maafisa 16 wa kaunti hiyo kwa tuhuma za ufisadi. Aidha Sang amelibuni jopo litakalochunguza madai ya ufisadi kisha kuwasilisha ripoti baada ya mwezi mmoja.

Aidha gavana huyo amewateua maafisa wengine kushikilia kikaimu wizara ambazo zimeathiriwa.

Hatua ya Gavana Sang inajiri siku moja tu baada ya maafisa tisa wa kaunti hiyo kukamatwa hapo jana kwa kupatikana na vifaa vya shule za chekechea na magurudumu tisini na tisa ya magari ya kaunti.