Waziri Mpya wa Elimu Profesa George Magoha, ameapishwa rasmi leo kuchukua hatamu ya uongozi katika wizara hiyo. Magoha ameapishwa mbele ya Rais Uhuru Kenyatta katika halfa iliyoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua.
Profesa Magoha sasa ana changamoto ya kuhakikisha mtaala mpya wa elimu unaokumbwa na pingamizi unatekelezwa. Ikumbukwe alipochujwa na Kamati ya Bunge ya Uteuzi alisema ana uzoefu mkubwa katika sekta ya elimu na yu tayari kwa utendakazi.
Kabla ya kuteuliwa kwa wadhifa huo, alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani, KNEC. Atakuwa waziri wa nne wa elimu chini ya utawala wa Rais Kenyatta baada ya mtangulizi wake, Amina Mohamed kuhamishiwa Wizara ya Michezo. Wengine ni Fred Matiang'i ambaye sasa ni Waziri wa Masuala ya Ndani ya Nchi. Jacob Kaimenyi alikuwa waziri wa kwanza wa elimu chini ya utawala wa Uhuru.