Na Sophia Chinyezi
Waziri wa Masuala ya Humu Nchini, Joseph Nkaissery ametetea ufaafu wa magari ya kivita yaliyonunuliwa na Idara ya Majeshi ya Ulinzi ya Kitaifa KDF kwa shilingi bilioni 1.1 kusaidia katika kukabili ugaidi. Waziri Nkaissery ameieleza Kamati ya Bunge ya Utawala na Usalama kwamba magari hayo yalifanyiwa majaribio kabla ya kununuliwa na kwamba yaliafikia viwango vya kimataifa. Rosa Agutu anakupasha.
Nkaissery alikuwa akijibu maswali ya wanachama wa kamati hiyo ambao awali walikuwa wameeleza wasiwasi kufuatia vifaa vilivyonunuliwa na serikali miaka miwili iliyopita.
Mbunge wa Ugunja, Opiyo Wandayi alimtaka waziri huyo kuwahakikishia wananchi kwamba magari hayo ni salama baada ya tukio la wiki iliyopita ambapo watu wanane wakiwamo maafisa saba wa polisi waliuliwa wakati gari lao lilipokanyaga kilipuzi Kaunti ya Lamu. Magari hayo thelathini yanadaiwa kununuliwa kisiri mwezi Februari mwaka uliopita kusaidia katika kukabili ugaidi na uhalifu.
Kadhalika, alitakiwa kufafanua sababu za kutaka bajeti ya ziada ya mabilioni ya pesa huku mwaka huu wa fedha ukitarajiwa kukamilika katika muda wa wiki tatu zijazo. Baadhi ya mapendekezo aliyotoa ni kwamba Wizara yake inahitaji shilingi bilioni mbili kuwashughulikia wakimbizi na bilioni nyingine bilioni 1.7 za shughuli za Tume ya Huduma za Polisi.
Wanachama wa kamati hiyo wameeleza wasiwasi kwamba iwapo bajeti hiyo itaidhinishwa, huenda ikasababisha utumiaji mbaya wa fedha za umma. Hata hivyo Nkaissery amesema fedha hizo ni za dharura kwa kuwa mbali na kushughulikia changamoto za kiusalama zinazoibuka. Bajeti hiyo ya ziada vilevile itasaidia kuwafidia wakimbizi wa ndani kwa ndani.