Na Mate Tongola Wakenya wanne wamewasilisha waraka wa kupinga uteuzi wa Askofu mstaafu Eliud Wabukhala kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya ufisadi EACC.  Wanne hao; Kasisi John Mbugua, Gilbert Mukabane, Eric Abu na Jeramba Munuhe wanadai kwamba Wabukhala alifeli katika utendakazi wake hivyo hastahili kuhudumu katika EACC. Katika waraka waliowasilisha bungeni wakati wa kikao cha kumhoji Wabukhala kilichoongozwa na Kamati ya Sheria na Haki ya Bunge la kitaifa, wanne hao wamemshtumu kwa kuwabatiza na hata kuwazika wahalifu jambo ambalo ni kinyume na maadili ya kikristo. Hata hivyo akijitetea, Wabukhala amesema ni jukumu la viongozi wa dini kutangamana na wenye dhambi ili kuwapa muongozo. Kamati hiyo ilimtaka kuelezea kuhusu mabadiliko atakayoteka katika EACC.  
Kamati hiyo itawasilisha ripoti yake kuhusu Wabukhala katika Bunge la Kitaifa tarehe kumi na saba mwezi huu wakati wa kikao maalum kilichoitishwa na Spika Justin Muturi. Wadhifa wa mwenyekiti wa EACC uliachwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa Philip Kinisu baada ya kuhusishwa na ufisadi.