Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Kimatibabu, KEMRI, Abdullahi Ali, amesema taifa lazima liimarishe matumizi ya data ya kuaminika, uwajibikaji, na hatua zilizoratibiwa ili kudhibiti tatizo la usugu wa dawa.
Akizungumza jijini Mombasa wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa wa Kenya wa AMR 2026, Ali alionya kuwa usugu wa dawa (antimicrobial resistance) – AMR ni tishio kubwa kwa utekelezaji wa mpango wa afya kwa wote, usalama wa afya ya taifa, maandalizi ya majanga ya kiafya, pamoja na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema kuwa AMR si suala la kisayansi pekee, bali pia ni changamoto ya utawala na sera inayohitaji uongozi thabiti, usimamizi endelevu, na utekelezaji madhubuti wa mikakati iliyopo.
Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika chini ya kauli mbiu “Data That Works: Working Together to Curb AMR in Kenya,” umewakutanisha watunga sera, wanasayansi, wahudumu wa afya, wasimamizi, na washirika wa maendeleo ili kutathmini hatua zilizopigwa na kuharakisha utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa AMR.
Daktari Ali alikiri kuwa Kenya imepiga hatua nzuri katika kuanzisha sera na mifumo ya kitaasisi ya kukabiliana na AMR, lakini akabainisha kuwa changamoto kubwa bado zipo, hasa katika ngazi za kaunti.
Alitaja ukosefu wa ufuatiliaji wa kutosha, matumizi madogo ya data ya AMR katika kufanya maamuzi, pamoja na uwajibikaji uliogawanyika kati ya taasisi mbalimbali, kama vikwazo vinavyoathiri ufanisi wa mapambano dhidi ya usugu wa dawa nchini.