Bwawa la ekari tano lililoko katika soko la Tala. [Patel Malevu, Standard]

Wakaazi wa Machakos wamepinga vikali mpango wa serikali ya kaunti hio wa kufukia bwawa la ekari tano lililoko katika soko la Tala ili kugeuza eneo hilo kituo cha magari ya uchukuzi wa umma.

Wakiongozwa na wakili Priscillar Kioko, John Mwangangi Mwovi, Sicas Sila Mutiso na Charles Kyalo, wakaazi hao wanasema bwawa hilo limekua lenye usaidizi mkubwa kwa jamii ya Tala kwa muda wa zaidi ya miaka 90 tangu lichimbwe.

James Mwovi Mwangangi alisema kuwa mpango huo wa serikali ya gavana Wavinya Ndeti ni kinyume na matakwa ya jamii ya ukambani na pia uliafikiwa pasi na mchango wa jamii.

"Eneo la ukambani ni eneo kame kutokana na mvua chache zinazoshuhudiwa, kinachosaidia ni mabwawa machache yaliyochimbwa likiwemo bwawa hili la Tala ambalo linatumika na wakazi wa maeneo ya Tala na Matungulu. Kamwe hatutakubali serikali ya kaunti kulifukia ilhali haijawai tuchimbia bwawa lolote" alisema Mwovi.

Kwa upande wake Charles Kyalo alimsuta mwakilishi wadi wa eneo hilo Jackson Ndaka akidai ndiye anayeshinikiza kufukiwa kwa bwawa hilo shutma zilizokaririwa na wakaaji wengine walioandamana naye kuhutubia wanahabari.

Akizungumza na radio maisha mwakilishi wadi huyo wa wadi ya Tala Jackson Ndaka alikiri kushinikiza hoja ya kufukiwa kwa bwawa hilo akidai ni ombi lililoketwa kwa ofisi yake na baadhi ya wakazi wa soko hilo la Tala.

“Bwawa hili la Tala limegeuka na kuwa tishio kwa afya na usalama wa wakazi. Hapa Tala hakuna mahali pa kuelekeza majitaka na karibu kila ploti hapa sokoni inaelekeza majitaka yake katika bwawa hili la Tala" alieleza Ndaka.

Kauli yake ilitiliwa mkazo na meneja wa manispaa hiyo ya Kangundo/Tala Justus Kiteng'u aliyetaja haja kwa jamii kushirikiana na viongozi kuboresha soko hilo la Tala

"Hoja ya kufukiwa kwa bwawa hilo haijatokana na afisi ya gavana Wavinya Ndeti ila ni pendekezo la baadhi ya jamii. Sisi kama serikali yetu ni kusikiliza uamuzi wa jamii na kutekeleza mapendekezo yao" Kiteng'u aliambia radio maisha katika mazungumzo sokoni Tala.

Hata hivyo jamii hiyo ya Tala kupitia kwa mmoja wao wakili Priscillar Kioko inataka badala ya bwawa hilo kufukiwa kutengenezwa kuwa kivutio cha kitalii.

"Ukielekea Machakos mjini kuna bwawa la Kamwilu, Oldonyo Sabuk kuna bwawa sisi hapa Matungulu hatuna chochote" alisema Wakili Kioko.