Polisi wakikabiliana na waandamanaji Picha: Hisani

Historia ya kweli ya Wakenya itaandikwa na Wakenya wenyewe. Leo nawaandikia wakenya hii barua na kuwaomba wasilie.

Msilie wazalendo wenzangu maana sote twajua kuwa nchi yetu inaumia, nchi yetu imebakwa na wezi wachache uongozini, nchi yetu sasa yatuhitaji sote tusimame kidete na kupinga dhulma hii.

Katika hii barua yangu kwenu nawaambie mapinduzi ya kukomboa Kenya yameanza rasmi sasa. Hii ni zamu ya kupendua uongozi fisadi, uongozi wa ukabila, uongozi wa chuki na wizi na kubadilisha na uongozi wa mapenzi. Uongozi wa serikali ya wote na sio serikali ya wawili.

Utawala wa Kenya ni dhalimu na ni muitifaki wa Uganda, Burundi, Rwanda, Congo miongoni mwa mataifa mengine yanayotawala raia wake kwa mabavu.

Utawala wa kuamini wao wakiua kwa sababu ya kupingwa au kuiba ni sawa. Utawala wa kihayawani uliojawa na chuki na ukabila. Utawala wa mtu mle mtu.

Leo uongozi wa Uhuru Kenyatta na William Ruto badala ya kutuahidi maendeleo ina tuahidi njaa, mahangaiko, ukabila, chuki, ufisadi, ukiritimba, huzuni na majonzi.

Uhuru Kenyatta na William Ruto sasa hawana jipya la kuwaeleza wakenya. Serikali ya wawili hawa haina tofauti na bata ambaye hata alishwe kokoto vipi bado atahara.

Kama ni kutunukiwa basi wawili hawa wanafaa watunukiwa nishani ya dhahabu kwa kuongoza Kenya na ufisadi, wizi wa mali ya umma, dharau, chuki, ukabila na ufisadi wa hali ya juu.

Wawili hawa sasa wanajipiga kifua na kuwatishia wakenya na semi zao za kutawala hadi mwaka wa 2022. Naandika barua hii kwa machungu ya jinsi ambavyo sisi sote wakenya tumebakwa na serikali fisadi zaidi Kenya.

Mwenzenu nalia, mwenzenu mie nimeamua kuwapa dosi ya ukweli leo. Msidanganywe eti mwanahabari hafai kuzungumzia siasa. Hii sio siasa bali ni maisha yetu. Leo katika barua hii tutaelezana ukweli bayana.

Leo Kenya Kenya yahitaji wakenya kujitolea na kupinga udhalimu huu wa hali ya juu. Wakenya wanafaa kuungana na kuondoa serikali fisadi uongozini. Mapinduzi ya mamoja, mapenzi dhidi ya chuki, umoja dhidi ya ukabila, uwiano dhidi ya mgawanyo, hii ndio dawa ya wezi wote Kenya uongozini mwaka wa 2017.

Msiogope serikali ya wezi, msiogope serikali ya chuki, msiogope serikali ya fitina, msiogope serikali ya ukabila. Wakija na silaha zao unganeni mje na silaha zenu za mapenzi.

Wakija na ukabila unganeni mje na ukenya, wakija na senti zao zisizo na adabu zileni na muwapake tope wakati wa uchaguzi.

Enyi wakenya msikubali kamwe akili ndogo kutawala akili zenu kubwa tena. Tumezoea dhihaka na matusi, tumepigwa asubuhi, mchana na usiku, kwa sababu sisi ni watu wa makabila tofauti, sisi tunapinga sera zao chafu, sisi hatukubaliani na wizi wao, sisi hatuwaabudu.

Tumeona ardhi yetu ikinajisiwa. Tumeona sheria zikitambua wenye nguvu na sheria tofauti kati ya watu wanyonge na watu wenye mihela.

Hatutasahau mamlaka zikijaza watu kwenye jela, kuanzia Mombasa, Wajir, Mandera, Bungoma, Mumias, Kisii, Kisumu, Garissa, Tana River, Muranga, Nyeri na kwengineko nchini.

Mamlaka ambazo sasa zinadaiwa kubaka kina mama na dada zetu wakitafuta bunduki zilizoibiwa huko Mumias, wakitafuta uwongo badala ya ukweli.

Hawa ni watu ambao hawakukubali kwamba haki ni ukandamizaji na unyonyaji. Hakuna mateso wala vitendo vyovyote vya kinyama vitakavyotufanya sisis kuomba huruma.

Ni bora tufe kwa heshima tukiamini kabisa na kujiamini kuhusu hatma ya nchi yetu kuliko kuishi kwenye utumwa na kuvunja misingi yetu.

Kuvunja heshima yetu na uzalendo wetu. Ipo siku historia itasema. Historia itakayofundishwa katika nchi zilizoondoa mabepari na wakabila wakubwa wa uongozi.

Kenya itaandika historia yake iliyojaa utu na heshima.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: mali@standardmedia.co.ke, FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter:
@mohajichopevu