Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir akiongoza shughuli ya ugavi wa chakula kwa watoto wa chekechekea. [Robert Menza, Standard]

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeimarisha juhudi zake za kuboresha elimu ya chekechea (ECDE) kwa kuwekeza katika lishe shuleni, ajira ya walimu na uboreshaji wa miundombinu, hatua ambazo zimeanza kuleta mabadiliko chanya kwa maelfu ya watoto kote kaunti hiyo.

Kupitia mpango wa lishe shuleni unaotekelezwa bila malipo, zaidi ya watoto 12,000 wanaosoma katika vituo vya ECDE wananufaika na chakula cha kila siku. Wadadau wa elimu wanasema mpango huo umeongeza mahudhurio ya wanafunzi na kupunguza visa vya utoro, hasa katika maeneo yenye familia zisizojiweza.

Wazazi na walimu wamesema kuwa upatikanaji wa chakula shuleni umeongeza motisha ya watoto kuhudhuria masomo kwa wakati na kubaki shuleni siku nzima. Aidha, hali ya umakinifu darasani imeimarika, jambo linalochangia matokeo bora ya ujifunzaji.

Ili kuboresha ubora wa elimu ya awali, Serikali ya Kaunti ya Mombasa imeajiri walimu 130 wa ECDE, hatua iliyolenga kupunguza uhaba wa walimu katika vituo vya umma na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani. Hatua hiyo imewawezesha walimu kuwafuatilia watoto kwa karibu zaidi katika hatua muhimu ya ukuaji wao.

Akizungumza kuhusu juhudi hizo, Gavana wa Mombasa, Abdulswamad Shariff Nassir, alisema kuwa mafanikio ya elimu ya awali yanategemea kutimizwa kwa mahitaji ya msingi ya mtoto.

“Mtoto mwenye njaa hawezi kujifunza. Tunapounganisha lishe bora, walimu waliohitimu na miundombinu imara, tunawaweka watoto wetu katika nafasi nzuri ya kufanikiwa,” alisema Gavana Nassir.

Kaunti hiyo pia inaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya ECDE kupitia mpango wa Ondoa Mabati, unaolenga kuondoa madarasa ya mabati na kujenga majengo ya kudumu na salama kwa watoto. Katika wadi ya Majoni, ujenzi wa kituo kikuu cha ECDE umefikia asilimia 80, huku miradi mingine ikiendelea katika maeneo mbalimbali ya kaunti.

Maafisa wa elimu wamesema kuwa mazingira bora ya kujifunzia ni nguzo muhimu katika kuimarisha ufaulu wa wanafunzi na ustawi wa walimu. Wataalamu wa elimu wamepongeza hatua hizo, wakisema kuwa mchanganyiko wa lishe shuleni, ajira ya walimu na uboreshaji wa miundombinu unaweka msingi imara wa mafanikio ya elimu ya muda mrefu, hasa kwa watoto kutoka familia zisizojiweza.