Wanafunzi wa shule ya msingi watembea kwenye barabara ilio jaa matope wakirejea nyumbani kutoka shuleni. [Collins Kweyu,Standard]

Shule nyingi nchini zinaendelea kufanya kazi huku zikiwa na idadi ndogo ya wanafunzi, na baadhi zikiripotiwa kutokuwa na mwanafunzi hata mmoja. Hali hii imeisukuma Wizara ya Elimu kuanza kuzingatia mpango wa kuziunganisha shule hizo na kuhamisha walimu kwenda katika taasisi zinazohitaji zaidi.

Katika ukaguzi wake wa hivi majuzi, wizara imebaini kuwa zaidi ya shule 6,000 zina wanafunzi chini ya 100, huku shule 10 za upili zikifungwa baada ya uchunguzi kubaini kutokuwa na wanafunzi kabisa. Hili limeibua maswali kuhusu uwezekano wa matumizi mabaya ya fedha za umma.

Shule 10 za upili zilizofungwa ni: Kiria (Nyandarua), Dr Machage Moheto (Migori), Ragia Forest High (Kiambu), Mugwandi Mixed (Kirinyaga), Friends Bulovi (Kakamega), Loiwat High (Baringo), Ngamba Secondary (Murang’a), Sintakara Secondary (Narok), Maji Mazuri Mixed (Baringo) na Fr Leo Staples Girls (West Pokot).

Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, alisema kuwa kati ya shule hizo, takriban shule 2,145 za msingi za umma zina chini ya wanafunzi 45 kila moja, huku shule 3,979 za sekondari za kidato cha chini (JSS) zikiwa na wanafunzi 90 au chini ya hapo.

Alisema uchunguzi unaendelea kubaini iwapo fedha zilikuwa zikitolewa kwa shule ambazo hazina wanafunzi, jambo ambalo linaashiria uwezekano wa uwepo wa “wanafunzi hewa”.

“Baadhi ya shule hizi zilikuwa na walimu lakini hazikuwa na wanafunzi. Tunachunguza ikiwa fedha ziliwahi kutolewa kwa shule hizi ili kubaini kama kulikuwa na udanganyifu. Ushahidi ukipatikana, tutawasilisha kwa uchunguzi wa jinai,” alisema Ogamba.

Wizara imezuia mgao wa fedha kwa shule ambazo taarifa zao za usajili wa wanafunzi hazijathibitishwa, kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kikisalia bila kutolewa.

Katika shule za msingi, wanafunzi 5,833,175 waliripotiwa katika shule 23,889, lakini ni shule 16,788 pekee zilizoidhinishwa kupokea mgao kamili. Shule 3,065 hazikuwasilisha data sahihi na zilipewa asilimia 50 tu ya mgao.

Katika shule za sekondari za kidato cha chini (JSS), idadi ya wanafunzi 2.43 milioni iliripotiwa awali, lakini baada ya uhakiki wanafunzi 2.94 milioni pekee katika shule 20,630 ndio waliostahiki fedha kamili. Shule 934 hazikupokea fedha kutokana na data potofu au kukosekana kwa taarifa.

Kwa sekondari za kawaida, wizara ilitenga shilingi bilioni 10.37 kwa wanafunzi milioni 3.35 katika shule 9,550. Baada ya uthibitisho, wanafunzi milioni 3.2 katika shule 9,540 walithibitishwa na kutengewa shilingi bilioni 10.09. Shule 10 zisizo na wanafunzi zilifungwa.

Waziri Ogamba alisisitiza kuwa wizara inalenga kuboresha uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali.

“Tunalenga kuhakikisha kuwa rasilimali tunazoomba na maamuzi tunayofanya yanalenga mahitaji halisi na yanategemea data sahihi na inayothibitishwa,” alisema.

Wizara pia imeahidi kuunganisha shule zenye idadi ndogo sana ya wanafunzi na kuwapangia walimu upya katika maeneo yenye mahitaji, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji ili kuzuia upotevu wa fedha kupitia wanafunzi hewa na shule ambazo hazipo.

Katika mgao wa muhula wa tatu, shilingi milioni 10 zilitengwa kwa elimu ya sekondari huru, shilingi bilioni 5.1 kwa sekondari ya chini, na shilingi bilioni 1.7 kwa elimu ya msingi, jumla ikiwa shilingi bilioni 16.5, huku shilingi bilioni 1 zikisalia bila kutolewa hadi uthibitisho ukamilike.

Waziri alihitimisha kwa kusema kuwa fedha zitatolewa tu kwa shule ambazo idadi ya wanafunzi wake imethibitishwa ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji.