Leo hii viongozi mbalimbali nchini na hata wa mataifa mengine wameshiriki Maombi ya Kitaifa awamu ya kumi na saba katika Hoteli ya Safari Park jijini Nairobi huku masuala mbalimbali yakiangaziwa yakiwamo upendo, amani, na ufisadi. Wabunge, wawakilishi wadi na waimbaji wamewatumbuiza wageni zaidi ya elfu tatu waliohudhuria kwa nyimbo aina aina. Rais Uhuru Kenyatta amesisitiza kwamba vita dhidi ya ufisadi vitaendelea bila kumsaza yeyote. Aidha Naibu wake William Ruto amejitetea dhidi ya kutoa michango makanisani kila uchao huku Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayadid akimwomba Rais kushirikiana naye katika kudumisha amani Sudan Kusini.
Viongozi mbalimbali waliopata fursa ya kuzungumza wamesisitiza suala la kulikabili ufisadi. Naibu wa Rais William Ruto, akizishauri idara za uchunguzi kuzidisha vita hivyo.
Aidha Ruto amejitetea dhidi ya tuhuma za kutoa michango makanisani. Amesema ataendelea kutoa michango hiyo akiwataka wanaomhusisha na wizi wa fedha za umma kukoma kufanya hivyo kwani hajahusika kwa vyovyote vile. Hata hivyo Spika wa Bunge la Kitaifa Justine Muturi amesema wanaotoa michango hiyo wanapaswa kuwajibishwa.
Viongozi hao wametoa hakikisho kwamba watashirikiana na idara za uchunguzi ili kuangamiza ufisadi. Hata hivyo, Rais Kenyatta amewasihi viongozi hao kudhihirisha kwa vitendo wanayosema.
Wakati uo huo, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir Mayadid, ameleeza imani kwamba amani itarejea katika taifa lake. Rais Kiir aidha amempongeza Rais Kenyatta kufuatia ushirikiano baina yake na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga. Amesema amani hudumishwa wakati upinzani unashirikiriana na serikali. Kiir amemwomba Rais kuingilia kati ili kurejesha amani Sudan Kusini. Rais Kenyatta ametoa hakikisho kwamba Kenya itashirikiana na taifa hilo katika harakati za kudumisha amani.
Awali hafla hiyo ilianza kwa maombi na nyimbo mwendo wa saa mbili asubuhi kaulimbiu ikiwa Mwamko Mpya kwa Taifa Letu.
Naye Spika wa Bunge la Seneti Ken Lusaka akawashauri viongozi kuhubiri amani miongoni mwa Wakenya hasa wanapokuwa katika mikutano ya hadhara.
Ikafika awamu ya wabunge kuwatumbuiza wageni.
Yakafuata maombi tena
Ikawa awamu ya Naibu Gavana huyo wa Kajiado kuongoza maombi.
Mwendo wa saa nne kamili, Mwimbaji Hellen Mtawali akawatumbuiza wageni kwenye wimbo ulioshamiri jumbe za amani, upendo na kukabili ufisadi.
Saa nne na dakika ishirini hivi, hotuba zikaanza huku Askofu Lord Michael Hesnis akizungumzia jinsi ya kuboresha uchumi wa taifa. Lord Hastine amemshauri Rais Kenyatta na viongozi serikali kuhubiri amani, kutubu dhambi zao wakati wowote ili kuiendesha serikali kwa njia ya busara.
Hafla hiyo imekamilika mwendo wa saa tano unusu, Spika Muturi akiwapongeza wote waliohudhuria.