Wafanyakazi nchini watalazimika kusubiri kwa muda zaidi kabla ya kujua iwapo wataongezewa mishahara au la. Ilitarajiwa kwamba huenda serikali ingetengaza nyongeza hiyo wakati wa maadhimisho ya Leba Dei. Hata hivyo, Waziri wa Leba Ukur Yattani aliyemwakilisha Rais Uhuru Kenyatta, amesema mazungumzo yatafanyika wiki hii baina ya serikali na washikadau mbalimbali kuhusu suala hilo suala ambalo limewaghadhabisha wafanyakazi.

Akihutubu wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi, Waziri wa Leba Ukur Yattani amesema mazungumzo hayo ndiyo yatakayobaini iwapo wafanyakazi wataongezwa mishahara au la.

Ni kauli ambayo inakwenda kinyume na tarajio la Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU ambao umekuwa ukiishinikiza serikali kutangaza nyongeza ya asilimia kumi na tano kwa mishahara ya wafanyakazi. Aidha Shirikisho la Waajiri FKE limekuwa likipinga mipango yote ya nyongeza ya mishahara likilalamikia kudorora kwa uchumi.

Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa COTU ameishtumu serikali kufuatia hatua yake ya kila mara kuwahangaisha viongozi wa miungano ya wafanyakazi, akiitaka kufuata taratibu zilizopo kisheria.

Kauli sawa na hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu KNUT Wilson Sossion, ambaye ameitaka serikali kuitekeleza mikataba yote ya utendakazi kabla ya

Viongozi hao wawili pia wameishtumu FKE kwa kususia hafla hiyo ya Leba dei na kuitaja kuwa isiyojali maslahi ya wafanyakazi.

Gavana wa Nairobi Mike Sonko, kwa upande wake ametoa wito kwa Serikali ya Kitaifa, kuongeza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti ili kuziwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo. Sonko amesema asilimia kumi na tano ya fedha wanazopokea kutoka kwa serikali hiyo ya kitaifa haitoshi, kwani sehemu kubwa ya pesa hizo hutumika katika kulipia mishahara ya wafanyakazi, huku kiasi kidogo kikisalia kwa maendeleo.

Amesema Kaunti ya Nairobi kwa mfano, inakabiliwa na changamoto za kifedha kutokana na kiasi kikubwa cha madeni yaliyorithiwa na mtangulizi wake.

Ili kukabili migomo ya mara kwa mara katika sekta ya umma hasa ile ya afya na elimu Waziri Yattani ametangaza mikakati mbalimbali iliyobuniwa ili kukabili tatizo hilo.

Maadhimisho ya leo yanajiri wakati ambapo mvutano unaendelea kushuhudiwa kuhusu kutekelezwa kwa ada ya asilimia 1.5 inayostahili kutozwa wafanyakazi na waajiri ili kufadhili ujenzi wa makazi yenye bei nafuu. Huku COTU ikisema kwamba itaunga mkono hatua iwapo tu, serikali itawaongeza mshahara wafanyakazi FKE imeapa kuendelea kupinga ikiitaja kuwa kinyume na sheria.