Skip to main content
× THE NAIROBIAN NAIROBIAN SHOP TEN THINGS HEALTH FLASH BACK FASHION MONEY ASIAN ARENA FEATURES TRAVEL UNCLE TED BETTING POLITICS Podcasts E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian Entertainment Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified Jobs Games Crosswords Sudoku The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
×
SPORTS

Wanasiasa wanafaa kufuata nyayo za hayati Rais Mwai Kibaki

BLOGS
By Ali Hassan | April 30th 2022 | 2 min read

Maisha haya maisha. Maisha ni ukungu! Ni kama mshumaa vile! Kila tunavyoishi ndivyo tunavyoisha.

Leo hii tupo pamoja tukipiga gumzo, tukicheka na kutabasamu, halafu ghafla bin vuu, jicho likipepesa tu, unasikia mwafulani katangulia mbele za haki.

Vifo vikiwa vya aina aina: majini, motoni, vitani, ajalini sikwambii maradhi. Wakifariki dunia watu wa sampuli sampuli: si mke si ndume; si wazee si vijana.

Yaani mauti hayachagui hayabagui. Ikifika nukta tu, malaika (Izraili) anakuja kutwaa roho. Siku si nyingi tangu nchi hii impoteze aliyekuwa rais wa awamu ya pili hayati mzee Daniel arap Moi.

Na sasa tena imo katika maombolezo baada ya rais wa awamu ya tatu, hayati mzee Emilio Stanley Mwai Kibaki kutuacha!

Hayati Kibaki amekuwa akiugua kwa muda, ijapo kimya kimya, tangu amemaliza mihula yake miwili ya uongozi. Ongezea na majonzi mengine yaliyompitikia mwaka 2016, kifo cha mkewe mama Lucy Kibaki.

Mengi yanasemwa kumhusu hayati Kibaki. Ijumaa wiki hii ni sikukuu ya kitaifa ili watu mbali mbali wajiunge na waKenya wa matabaka mbalimbali kumwomboleza hayati Kibaki, na kumfanyia maombi (misa) maalum kabla ya mwili wake kufukiwa mchangani huko Othaya, Nyeri, Jumamosi hii.

Hayati Kibaki, aliyezaliwa mwaka 1931 na kutuacha mkono mwaka 2022, ameyapitia, kuyaona, kuyasikia na kuyafanya mengi mno katika nyanja mbali mbali.

Achia mbali longolongo za mwanasiasa yeyote yule, hayati Kibaki ameondokea kuwa mtu ambaye aliheshime kauli na miungano na wanasiasa wengine. Hii ni kwa mujibu wa ushahidi unaotoka kwa wanasiasa wengineo kumhusu hayati.

Akifariki dunia mtu inakuwa vema kusemwa kwa uzuri; wanasema wanadini. Ingawa hivyo, mauti yanatufunza mambo mengi tu. Mathalan, anajitokeza mwanasiasa na kumtaja hayati Kibaki kama mwanasiasa/kiongozi aliyependa raia wake, hakuwa mwizi, hakutukana mtu (malaika nini?), na bla bla bla nyingi tu. Halafu huyo, keshoye, anasikika akitukanana, au akiwa kizimbani kwa tuhuma za wizi! Hatujifunzi jamani.

Subira aliokuwa nayo hayati Kibaki ni ya kupigiwa mfano. Akigombea urais na kubwagwa. Akidondoshwa kutoka katika wadhfa wa Makamu Rais lakini asizue makeke!

Na kama alivyo binadamu yeyote yule, hakuna mja mkamilifu.

Hayati Kibaki ameondoka duniani na kovu la mauaji na uharibifu wa mali kufuatia zogo la baada ya uchaguzi mkuu ulioandaliwa mwaka 2007; misukosuko ya hapa na pale ya serikali mahuluti aliyobuni na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga; vipi kuhusu sakata za  Anglo-Leasing na Goldenberg?

Sasa hivi tunaelekea katika kipindi kigumu mno. Uchaguzi mkuu, Agosti 9. Amesifiwa mno hayati Kibaki kwa kuimarisha uchumi wa nchi.

Je, wanasiasa hao ambao sasa hivi wapo katika kinyang’anyiro cha nyadhfa mbali mbali, wataimarisha uchumi au zao ni hekeya tu za Alfu Lela Ulela?

Je, ucheshi wake hayati Kibaki kwenye semi zake na hotuba zake, vikiwepo vimbwanga vya kuvunja mbavu, vitaigwa na wanasiasa wa sasa au vitazalisha hotuba za chuki na uchochezi punde baada ya hayati Kibaki kufukiwa mchangani?

Sasa hivi wasikilize wanasiasa wanavyonyenyekea kwa kumsifu hayati Kibaki. Wengine wamesitisha safari zao, kampeni zao, shughuli zao, almradi wamuomboleze hayati Kibaki. Lakini wafuate baada ya mazishi ya hayati Kibaki! Ole wetu!

Maskini binadamu alivyo msahaulifu kama kuku ambaye anatoroka na kufurahikia tonge lililochovywa kwenye mchuzi wa kuku mwenziye aliyechinjwa!

[email protected]

Share this story
Princess Hotel where Kibaki took Lucy for dates now mute
Many people still come asking for ‘Princess’. The joint was famous because prominent politicians used to frequent it before independence
Lesson from Kibaki: Money must be worked for, not given for free
His motto was simple: “If you think I will be a good leader, a good mhesh, then just vote for me. But if it is about freebies, utatembea.” 
.
RECOMMENDED NEWS
Feedback