Moha Jicho Pevu: ICC- Waathiriwa walijiua wenyewe

Kesho(yani tarehe 16 mwezi huu) vyombo vyote vya habari vitaangazia sherehe ya Uhuru Kenyatta na William Ruto katika uwanja wa Afraha Nakuru.

Kilele cha sherehe ya ushindi wao dhidi ya mahakama ya jinai huko Uholanzi, Hague, itakuwa ni hotuba ya wawili hao.

Wanahabari kahawa watapachika kamera zao katika kila kona kupeperusha matangazo hayo moja kwa moja kutoka uwanja huo.

Nawaita wanahabari kahawa kwa sababu chai walioinywa katika ikulu ya Nairobi iligeuza fikra zao na taaluma na kuwafanya wanahabari wa kutangaza sifa, mavazi na makalio ya wanawake. Siku itakayofuatia, baada ya sherehe hizo, magazeti za humu nchini zitatwaa picha za wawili hao na kuwafananisha na mashujaa licha ya wao kujua wazi kuwa huo utaonekana kama kejeli kwa wakenya na familia za waathiriwa wote wa ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007.

Kesho wanahabari watawasahau kina mama waliobakwa, kina mama na watoto walioteketezwa ndani ya kanisa la Kiambaa na familia moja iliyopigwa moto ndani ya nyumba yao huko Naivasha.

Mauaji sugu kule Kibera, Mombasa, Kisumu na Bonde la Ufa miongoni mwa maeneo mengine yalioathirika wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi pia yatasahaulika.

Nakuru ndio utovu wa unyama huo na kesho mpira utageuzwa baada ya miaka tisa ya kutafuta haki na kuishia miaka tisa ya sherehe.

Kabila mbili zilizochukiana na kuuana kinyama kesho zitaonana nakujifanya kuwa hamna chochote kilichotokea mwaka wa 2007 licha ya kuangaliana na jicho la tatu la hasira.

Viongozi mbali mbali wa ‘dini senti’ watafika katika uwanja huo — sio kumsifu Mungu. Naam, wamekuwa watu wa kuhubiri meno badala ya neno.

Kitendo hiki kinaashiria kwa kifupi kuwa zaidi ya wakenya elfu moja waliouawa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi walijiua wenyewe, na kwa hiari yao. Walitaka kubakwa wenyewe kwa hiari yao, walitaka kufumwa mishale kwa hiari yao, walitaka kuchomwa kwa hiari yao, walitaka kukatakatwa kwa mapanga kwa hiari yao.

Jameni ni nani aliyeturoga? Mwataka kuniambia waliochomwa ndani ya kanisa ya kiambaa hawana haki? Je, makosa yao ni kuwa maskini? Mbona ukiritimba huu wa maskini akifa hana faida unazidi kuwaandama?

Je, mnaokwenda kuhudhuria mkutano huo, huku mkiimba nyimbo za kumsifu Mungu, hamuogopi? Hamuogopi Mungu japo kwa sekunde?

Endeleeni maana Kenya mungu wake ni ukabila, endeleeni lakini mkae mkijua Mungu ndiye Mkuu na kwake haki itapatikana.

Sisemi ni makosa kuhudhuria sherehe hizo. La hasha! Ninachosema ni kuwa hatuwezi sherehekea uhuru wa watu wawili dhidi ya haki ya watu zaidi ya elfu moja. Tabia hii inanikumbusha maandiko ya ndugu zangu wakristo pale Pilato aliponawa mikono yake na kuamua kuuawa kwa Yesu na kuachiliwa kwa Barnabas. Hii ndio Kenya ya sasa. Kenya ya kutaka kila doa la uongozi kuanzia chifu wa mtaa kuteuliwa kuwa Barnabas huku wale wasafi wakipakwa topwe na kutusiwa kila kukicha maana wamekataa kula na kulala na wezi.

Lau kama mkutano huo ungelikuwa wa kuwaombea waathiriwa wa ghasia hizo, hakika pia mimi ningelifunganya safari na kuhudhuria kwani niliyoyaona mwaka wa 2007 bado yamo akilini mwangu. Ghasia hizo zilifanya wengi wetu wanahabari kuweza kupata ushauri wa nasaha kutoka kwa wanasaikolojia kwani idadi kubwa ya walioangazia ghasia hizo walikuwa hawajielewi kutokana na yale waliokumbana nayo.

Enyi wakenya wakabila nambari moja, kaeni mkifahamu kuwa Kenya ina shida ya uongozi, kaeni mkijua kuwa Kenya mahakama zake zimebakwa, kuwa Kenya hamna bunge — iliyopo ni bunge la mafisi wanaofyonza damu ya wakenya — kaeni mkijua kuwa hamna cha ICC tena.

Kenya sasa ni sawia na riwaya ile ya Shamba la Wanyama ambapo ingawa wanyama wote ni sawa, kuna wengine bora zaidi ya wengine. Sherehe ya kesho inadhihirisha riwaya hiyo na kutamatisha na ile ya AME na ZIDI yaani AMEZIDI.

Hakika sisi wakenya tumezidi. Tumezidi na kujawa na uozo wa kutotaka kutafuta haki.

Taifa hili limekuwa la matajiri. Na huku mkiendelea kusheherekea msisahau kuwa katika kaunti hiyo hiyo, watoto 39 tayari wamekufa kutokana na homa ya mapafu.

Walakin kwa sababu ni watoto wa maskini, hamna mtu aliye na haja dhidi yao. Wanahabari pia watakuwa na muda mwingi wa kuangazia sherehe kwa sababu watoto waliokufa hawawezi tatiza sherehe hizo.

Nina machungu kila nikikumbuka vilio vya kina mama na watoto katika uwanja wa maonyesho ya ukulima ya Eldoret. Nina machungu nikiona kejeli hii lakini Mungu ni Mkuu na hakika atawalipia wote walioathirika katika ghasia hizo. Poleni nyote wana-2007. Mungu ailaze roho yenu mahala pema panapolazwa wema.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN.

Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter:@mohajichopevu

By AFP 4 hrs ago
Athletics
Beijing half marathon runners stripped of medals after controversial finish
By AFP 16 hrs ago
Football
Arsenal, Liverpool fight to keep Premier League race alive
Athletics
World hammer silver medallist Kassanavoid eyes glory at Nyayo on Saturday
Athletics
Eldoret City Marathon to have a bigger 10km fun run