×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Chama cha Wafanyakazi, chalalamikia mazingira duni ya kudanyia kazi kwa wahudumu wa afya

Chama cha Wafanyakazi, chalalamikia mazingira duni ya kudanyia kazi kwa wahudumu wa afya

Siku moja tu baada ya Radio Maisha kuangazia masaibu wanayopitia wagonjwa na wahudumu wa afya katika Hospitali ya Saboti, Kaunti ya Trans Nzoia, sasa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika kaunti hiyo Samuel Kiboi ameishtumu serikali ya kaunti kufuatia mazingira duni ya kufanyia kazi hospitalini humo.

Katika taarifa, Kiboi amesema wahudumu wa afya hawana vifaa vya matibabu hali inayolemaza kabisa utoaji huduma kwa wagonjwa.

Aidha, Kiboi amesema wahudumu hao wako kwenye hatari ya kuambukizwa virusi vya korona iwapo serikali hiyo haitazingatia maslahi yao. Amekariri kwamba ilivyo sasa, wahudumu hao hawana maski na vifaa vya kupima virusi vya korona.

Kadhalika amedokeza kwamba hospitali hiyo haina ambulensi ya kuwasafirisha wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura.

Pia amelalamikia ukosefu wa dawa hospitalini humo, jambo ambalo limewalazimu wagonjwa kutafuta huduma katika hospitali za binafsi.

Wakati uo huo, Kiboi amesikitishwa na hali ngumu wanayopitia akina mama wajawazito. Amesema kuwa serikali haijakuwa ikituma pesa Linda Mama hasa baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha sheria inayoruhusu Wizara ya Afya kusimamia kitengo hicho. Amesema kuna uhaba mkubwa wa taulo na vitanda huku wakilazimika kulala sakafuni wakati mwingine.

Kadhalika vyoo vimejaa hospitalini humo, hali inayotishia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu. Vilevile ameilaumu Wizara ya Afya kwenye kaunti hiyo kufuatia utepetevu.

Jana, mmoja wa wahudumu wa afya aliiambia Radio Maisha kwamba juhudi zao za kutaka hali kuboresha zimegonga mwamba. Alisema kwamba wahudumu hawana glavu, sare rasmi huku wakilazimika kuvaa maski kwa zaidi ya siku mbili. Mhudumu  pia alisema kwamba wagonjwa wanalazimika kununua dawa madukani. Aliilaumu Serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia kwa kuwatelekeza.

Share this: