×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Rais afungua kaunti za Nairobi, Kajiado, Nakuru, Kiambu na Machakos

Rais afungua kaunti za Nairobi, Kajiado, Nakuru, Kiambu na Machakos

Rais Uhuru Kenyatta ameondoa marufuku ya kutoka na kuingia katika kaunti tano zilizokuwa zimefungwa ambazo ni Nairobi, Nakuru, Kajiado, Kiambu na Machakos.

Haya yanajiri mwezi mmoja tu baada ya Rais Kenyatta kusitisha safari za kuingia na kutoka kaunti hizo tano ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya korona ambayo yalikuwa yakiongezeka kwa kasi.

Katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya Siku ya Leba katika Ikulu hapa jijini Nairobi, Rais pia ametangaza kuwa marufuku ya kuwa nje yataanza kutekelezwa kuanzia leo hii saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri, tofauti na awali ambapo yalitekelezwa saa mbili usiku hadi saa kumi alfajiri.

Marufuku ya kuwa nje saa mbili hadi saa kumi alifajiri yalitekelezwa katika kaunti hizo tano pekee, maeneo mengine yakianza saa nne hadi kumi alfajiri.

Aidha, wamiliki wa mikahawa wamepata afueni katika kaunti hizo tano baada ya Rais kuruhusu mikahawa na hoteli kufunguliwa tena.

Hata hivyo, wamiliki wa mikahawa na hoteli wametakiwa kuhudumu hadi saa moja jioni kwa kuzingatia masharti ya kudhibiti maambukizi.

Baa vilevile zitahudumu hadi saa moja jioni.

Maeneo ya kubudu vilevile yameagizwa kufunguliwa, huku thuluthi moja pekee ya waumini wakiruhusiwa kuhudhuria ibada.

Marufuku ya mikutano ya kisiasa yataendelea kutekelezwa hadi wakati usiojulikana.

Pia Rais ameagiza waajiri kuwaruhusu wafanyakazi walio na umri wa miaka hamsini na minane na zaidi kufanyia kazi nyumbani.

Aidha, wafanyakazi katika taasisi za umma na binafsi wametakiwa kuzingatia umbali wa mita moja unusu katika ofisi zao.

Wafanyakazi wanaotoa huduma maalumu pekee ndio wametakiwa kuwa kazini ila kwa kufuata maagizo ya Wizara ya Afya.

Uhuru pia ametangaza kwamba shule zitafunguliwa jinsi ilivyopangwa na Wizara ya Elimu.

Tangazo hilo limewaondolea wanafunzi hofu kwani wengi walikuwa na wasiwasi kwamba huenda wangesalia nyumbani hasa wakati huu taifa linapokumbwa na wimbi la tatu la Korona.

Vilevile Kenyatta ametangaza kurejelewa kwa hafla za michezo ila mwongozo wa kufuatwa utatolewa na Wizara ya Michezo.

Hata hivyo, Rais ameonya kwamba yeyote atakayekiuka masharti ya kudbibiti maambukizi ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema atalazimika kuweka masharti zaidi iwapo maambukizi ya korona yataongezeka tena.

Haya yanajiri wakati ambapo wanaharakati walikuwa wamepanga maandamano hadi Ikulu kulalamikia masharti makali ya kudhibiti maambukizi bila mikakati ya kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Wanaharakati hao walimshtumu Rais kufuatia masharti hayo ambayo wanasema yamesababisha kudorora kwa uchumi huku Wakenya wakiendelea kuteseka.

Hata hivyo, polisi waliingilia kati maandamano hayo kwa kuwarushia vitoza machozi.

Share this: