
Mipango ya mazishi ya Mbunge wa Bonchari John Ororo Oyioka inaendelea nyumbani kwake katika Kaunti ya Kisii.
Maafisa wa Tume ya Huduma za Bunge PSC na wabunge kumi na wanane wamefika katika boma la Oyioka na kukagua jinsi shughuli hiyo inavyoendeshwa kwa ushirikiano na Kamati-Andalizi ya familia ya marehemu.
Viongozi hao aidha wamekagua Uwanja wa Shule ya Upili ya Itierio ambapo ibada ya mazishi itafanyika vilevile Uwanja Mdogo wa Ndege wa Suneka.
Aidha wamefanya mkutano na maafisa wakuu wa usalama katika eneo hilo wakiongozwa na Naibu Kamishna.
Akizungumza na wanahabari, Mbunge wa Mugirango Kaskazini Joash Nyamoko amesema ibada ya mazishi itafanyika kuambatana na utaribu wa mazishi ya maafisa wa serikali, hasa wabunge.
Mwili wa Mbunge Oyioka ambaye alifariki Jumatatu wiki jana, unatarajiwa kuzikwa Ijumaa wiki hii, huku viongozi mbalimbali wakitarajiwa kuhudhuria.
Share this: