
Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC imesema inazichunguza kaunti tano kuhusu jinsi zilivyotumia mamilioni ya fedha wakati maambukizi ya virusi vya korona yalikuwa yamezidi nchini.
EACC imesema inalenga kufahamu jinsi fedha zilivyotumika katika shuguli za ununuzi, utoaji tenda na uajiri wakati wa kipindi hicho.
Tayari Mkaguzi Mkuu wa Serikali amezitaja baadhi ya kaunti zinazosemakana kutumia visivyo pesa za umma kununua dawa na vifaa vya kujikinga dhidi ya korona. Miongoni mwa kaunti hizo ni Bungoma, Kakamega, Kericho, Kiambu, Kisii, Kisumu na Laikipia.
Mkurugenzi mkuu wa EACC Twalib Mbarak, amesema uchunguzi wao wa awali umebainisha kwamba kulikuwapo na ukiukaji mkubwa wa sheria wakati wa ununuzi na utoaji tenda hatua zilizosababisha kupotea kwa mamilioni ya pesa.
Wakati uo huo, amesema ufisadi umekithiri zaidi katika baadhi ya taasisi za umma huku akiwakosoa wananchi kwa kuchangia hali hiyo.
Kuhusu sakata ya Mamlaka ya Ununuzi na Usambazaji Dawa KEMSA, Twalib ameitetea EACC akisema ilikamilisha uchunguzi wake na kuwasilisha faili kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma DPP.
Amesema ana imani kwmaba DPP pia anaendeleza uchunguzi wake kuhakikisha kwamba ana ushahidi wa kutosha kabla ya kuwasilisha kesi hiyo mahakamani.
Ameyasema hayo wakati wa mkutano na wanahabari mjini Naivasha baada ya kukamilika kwa mafunzo kuhusu ufisadi mwa maafisa wa KDF.
Share this: