
Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC inaendelea na uchunguzi kufuatia tuhuma za ufisadi zinazohusu kampuni ishirini na tano za mawakili akiwamo Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang'ata.
Aidha, Kampuni ya Mbunge wa Makueni Dan Maanzo, vilevile ipo miongoni mwa kampuni hizo za mawakili zinazohusishwa na madai ya wizi wa mamilioni fedha kutoka serikali ya Kaunti ya Nairobi kwa kipindi cha miaka saba iliyopita
EACC inachunguza malipo ya huduma za mawakili katika kampuni hizo kuanzia mwaka wa 2013 hadi mwaka wa 2020, kwa madai kwamba malipo hayo yamekuwa yakitolewa kinyume na sheria.
Kupitia barua yake kwa mawakili hao akiwamo Kang'ata ambaye pia ni Seneta wa Murang'a, EACC imeagiza washukiwa wote kuwasilisha risiti za malipo ili kufanikisha uchunguzi huo.
Mwaka wa 2019, Kamati ya Uhasibu katika Bunge la Nairobi ilifichua kwamba Idara ya Sheria ilikuwa imetumia zaidi ya shilingi milioni mia nne na themanini katika kulipia kesi mbalimbali, kinyume na shilingi milioni mia moja pekee ambazo hutengwa kwa ajili ya shughuli za kisheria.
Hata hivyo, Kang'ata amekashifu hatua ya EACC akisema ni mbinu ya watu fulani serikalini kutaka kumkandamiza kisiasa.
Kang'ata anasema aliwakilisha Serikali ya kaunti ya Nairobi mahakamani katika kesi moja mwaka wa 2018, na kwamba alilipwa baada ya kutoa huduma zake jinsi inavyohitajika kisheria.
Haya yanajiri wiki chache tu baada ya Kang'ata kumtumia Rais Uhuru Kenyatta barua ya kumfahamisha jinsi umaarufu wa BBI unavyopungua nchini hasa katika eneo la Mlima Kenya, ambako kumekuwa kukifikirika kuwa eneo lenye ufuasi mkubwa wa rais.
Share this: