
Siasa za eneo la Magharibi zimeendelea kuchacha huku Seneta wa Kakamega Cleophas Malala akimhimiza Kinara wa ANC Musalia Mudavadi, kutokubali kushurutishwa kumuunga mkono mgombea mwengine wa urais mwaka wa 2022.
Akizungumza katika mazishi kwenye eneo la Khwisero katika kaunti ya Kakamega, Seneta Malala amesema Kinara wa ODM Raila Odinga anapanga kuwania urais baada ya kuungwa mkono na vigogo wa muungano wa NASA, hivyo kumshauri Mudavadi kujiepusha naye ili kulenga kuwania urais.
Hata hivyo, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya amepuuza kauli ya Malala akisema Odinga hajatangaza kwamba atawania urais mwaka wa 2022 licha ya kuwa kiongozi wa ODM.
Wakati uo huo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi COTU, Francis Atwoli, amekariri kwamba Jamii za eneo la Magharibi zimeungana, na kwamba kusema jamii hizo zimesambaratika kisiasa ni dhana potovu.
Kwa upande wake Mudavadi, ameeleza haja ya serikali kudumisha uhuru wa Idara ya Mahakama nchini, na kwamba utendakazi wa mahakama unategemewa na sekta mbalimbali katika kufanikisha maendeleo.
Share this: