
Mchakato wa kumchagua Jaji Mkuu mpya umeanza rasmi baada ya Tume ya Huduma za Mahakama, JSC kutangaza kuwa wazi wadhifa wa Jaji Mkuu baada ya David Maraga kustaafu.
Kupitia notisi katika Gazeti rasmi la Serikali, Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu ametangaza kuwa wazi nafasi hiyo na sasa kupisha shughuli za kuwasajili wanaolenga kuchukua wadhifa huo.
Jaji mkuu mpya na watatu chini ya Katiba ya mwaka wa 2010 atapokea mshahara kati ya shilingi elfu mia tisa na milioni 1.3 kwa mwezi.
Anayetaka kuwania, lazima awe na tajriba ya miaka kumi na mitano kama jaji wa mahakama kuu ama ya rufaa, mwadilifu na atakayetekeleza wajibu wake pasi na miegemeo.
Wanaopigiwa upatu kuchukua nafasi hiyo ni Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, Jaji wa Mahakama ya Juu Smokini Wanjala, mwenzake Njoki Ndung'u na Isaac Lenaola.
Wengine ni Rais wa Mahakama ya Rufaa Jaji William Ouko, Jaji wa Martha Koome, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kihara Kiriuki, Profesa Githu Muigai, aliyekuwa Mbunge wa Mandera ya Kati Wakili Abdkadir Mohammed na Philip Murgor.
Hata hivyo, matarajio ya wengi ni kwamba atakayetwaa wadhifa huo hatakuwa kikaragosi wa serikali na kwamba ataiga mifano iliyotolewa na Maraga ambaye alisimama kidete katika maamuzi yake na kuu zaidi kutetea pakubwa kutekelezwa kwa katiba kikamilifu.
Share this: