
Siasa za Useneta wa Machakos zimesheheni kwenye makanisa mbalimbali katika Kaunti ya Machakos ambapo viongozi wa kisiasa wa eneo la Ukambani wameandamana na wanaogombea wadhifa huo kwa lengo la kuwapigia debe.
Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka akiandamana na mgombea wake Agnes Kavindu Muthama katika Kanisa la AIC Kasina, ameeleza kuwa alimchagua Kavindu kwa kuwa ana imani kwamba ana uwezo wa kuwatetea wakazi wa Machakos, na wala si kukabiliana na aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama jinsi ambavyo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakidai.
Mbunge wa Kangundo Fabian Muli wa Chama cha GDDP ameandamana na Simon Kitheka anayegombea wadhifa huo kwa tiketi ya chama hicho, wamehudhuria ibada katika Kanisa la ABC Bomani Mjini Machakos, ambapo amewasihi wakazi kumuunga mkono Kitheka.
Kwa upande wa Chama cha Maendeleo Chap Chap kikiongozwa na Naibu Gavana wa Machakos Francis Maliti wamempigia debe mgombea wao kwa jina Mutua Katuku katika kanisa Katoliki la Matuu kwenye eneo la Yatta, ambapo wamewasihi wapiga kura kuunga mkono chama kilichoanzishwa na mkazi wa Machakos.
Viongozi wote hao wanaonekana kuanza sera zao mapema hata kabla ya kutangazwa kwa muda rasmi wa kampeni kuwatambulisha wagombea wao kwa wakazi. Agnes Kavindu ni mgombea wa Chama cha Wiper.
Wengine wanaogombea wadhifa huo ni Urbanas Ngengele wa chama cha UDA, Lily Nduku wa CCU na wengine wagombea huru.
Share this: