
Naibu wa Rais, William Ruto ameendelea kusuta Chama cha Jubilee akisema kimeingiliwa na watu mbalimbali kiasi cha kusambaratika na kushindwa kuwateua wawaniaji wa viti kwenye chaguzi ndogo zinazotarajiwa.
Kauli ya Ruto imejiri baada ya Jubilee kutangaza kwamba haitakuwa na wawaniaji kwenye maeneo ya Machakos, Kabuchai na Matungu ili kuachia vyama vilivyoko katika muungano wa NASA kuwateua wawaniaji kwani waliokuwa viongozi wa maeneo hayo walikuwa wanachama wa muungano huo.
Aidha, Ruto amerejelea kauli yake ya kumkosoa Rais Uhuru Kenyatta ya kusema wakati umewadia wa kuyapa nafasi makabila mengine kuongoza taifa akisema viongozi wanastahili kuchaguliwa kwa kuzingatia sera zao wala si kabila.
Wakati uo huo, Ruto ameendeleza shutuma dhidi ya Kinara wa ODM, Raila Odinga, akisema kuna masuala mengine yanafaa kufanywa kipaumbele ukiwamo uchumi badala kuifanyia katiba marekebisho.
Ruto ameyasema hayo akiwa Mjini Bomet baada ya kukutana na Kiongozi wa Chama cha Mashinani CCM Isaac Ruto, aliyekuwa Gavana wa Bomet na Mshirika wa Odinga.
Share this: