
Tume ya Uchaguzi IEBC imejitetea dhidi ya madai yaliyoibuliwa Kamati ya Kiufundi ya Mpango wa BBI kwamba inajikokota katika kuthibitisha saini ilizowasilisha kwake, ili kufanikisha kufanyika kwa kura ya maamuzi.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema shughuli ya kuthibitisha saini hizo imeanza katika ukumbi wa Bomas.
Chebukati amesema IEBC imekodi eneo hilo rasmi kwa shughuli hiyo na kwamba ina vifaa vya kutosha kinyume na ilivyodaiwa na kamati hiyo ikiongozwa na Mbunge wa Suna Junet Mohamed. Amesema japo kumekuwapo na changamoto ya mtandao haijaathiri shughuli nzima.
Ameahidi kwamba shughuli hiyo itakamilika haraka iwezekanavyo.
Taarifa hii imejiri siku moja tu baada ya Kamati hiyo kutoa makataa ya siku kumi na sita kwa IEBC kukamilisha mara moja shughuli za kuthibitisha saini hizo.
Junet alidai kuwa kufikia Ijumaa wiki iliyopita, takriban saini elfu mia tano arubaini pekee zilikuwa zimethibitishwa na makarani wa tume.
Share this: