
Wizara ya Elimu imewaagiza walimu wakuu kutowaruhusu wanahabari kuangazia hali ilivyo kwenye taasisi hizo.
Katika baadhi ya maagizo kwa wakuu hao ambayo tumefanikiwa kuyadurusu, walimu wakuu wametakiwa kuhakikisha hakuna mikusanyiko ya watu shuleni vilevile kutowaruhusu wanahabari huku wakiarifiwa kwamba taarifa zozote kuhusu hali shuleni zinastali kutolewa na Waziri wa Elimu, katibu wake vilevile Katibu wa Tume ya Huduma za Walimu, TSC.
Uhalisia wa agizo hilo umedhihirika kwenye Kaunti ya Busia ambapo Mkurugenzi wa Elimu ametoa agizo kwa walimu wakuu kutowaruhusu wanahabari shuleni. Agizo sawa la hilo vilevile limetolewa na Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Pokot Magharibi, Jacob Onyego.
Ikumbukwe vyombo vya habari vimekuwa vikiangazia hali katika shule mbalimbali hasa mikakati iliyowekwa ili kuzuia maambukizi ya virusi vya korona huku ikibainika kwamba shule nyingine hazina mazingira ya kuridhisha kwa wanafunzi kusomea.