
Rais Uhuru Kenyatta amepiga marufuku shughuli zote za michezo, mashindano ya mziki vilevile hafla za kuwazidi wanafunzi shuleni kwa muda wa siku tisini zijazo baada ya shule kufunguliwa.
Katika agizo la Rais ambalo limetolewa leo hii wakati wa kikao na Kamati inayoshughulikia Kufanikisha Kufunguliwa kwa Shule, Rais Uhuru Kenyatta aidha ameongeza muda wa kutekelezwa kwa amri ya kutokuwa nje kati ya saa nne usiku na saa kumi alfajiri hadi tarehe kumi na mbili mwezi Machi.
Aidha amewataka viongozi wa kidini kuendelea kuhakikisha kuwa masharti ya awali ya kukabili korona kwenye maeneo ya kufanya ibada yakiwamo makanisani na misikitini kuendelea kutekelezwa.
Wakati uo huo Rais ameagiza kuendelea kutekelezwa kwa marufuku ya mikutano yote ya kisiasa huku akiwahimiza wanaoandaa hafla za harusi na mazishi kuhakikisha kuwa wanafuata agizo la kuhudhuriwa na watu mia moja hamsini pekee.
Kuhusu uchukuzi, Rais Kenyatta amewataka abiria wote vilevile watumiaji wa magari binafsi kuhakikisha wanavaa maski kila wakati vilevile kubeba asilimia sitini ya abiria wa kawaida.
Aidha wasimamizi na wazazi wameshauriwa kutowatembelea wanao shuleni iwapo hapana sababu za kimsingi huku walimu walio na zaidi ya umri wa miaka hamsini na minane wakitakiwa kuwa makini wanapoyatekeleza majukumu yao.
Walimu wakuu vilevile wametakiwa kuwatambua wanafunzi wanaougua magonjwa mengine sugu na kuhakikisha hali zao za kiafya zinafuatiliwa mara kwa mara na maafisa wa afya katika ngazi ya kaunti.
Share this: