
Tume ya Huduma za Walimu, TSC imewaagiza maafisa wake wote walio katika likizo kurejea kazini mara moja ili kufanikisha mchakato wa kufunguliwa kwa taasisi za elimu Januari 4.
Katika waraka uliotumiwa wakurugenzi wote wa TSC kwenye kaunti, wametakiwa kuhakikisha masharti ya kuzuia maambukizi ya virusi vya korona yanazingatiwa katika taasisi zote za elimu zitakapofunguliwa.
Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Nancy Macharia amesema kwamba tume hiyo imebuni kundi la dharura la kushughulikia masuala ya korona ambalo litakuwa na jukumu la kukusanya taarifa kutoka kwa maafisa wake kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhusu hali ilivyo hasa masomo yatakaporejelewa kwa ukamilifu.
Aidha, walimu wakuu wa shule wamtakiwa kuhakikisha wanabuni makundi ya kulishughulikia janga la korona yatakayowajumuisha watu watano katika kila shule. Miongoni mwa watu hao ni walimu wawili, mwanachama mmoja wa bodi ya usimamizi wa shule, mfanyakazi mmoja wa shule ambaye si mwalimu na mwanafunzi mmoja.
Share this: