
Uchaguzi mdogo wa Ugavana kwenye Kaunti ya Niarobi utafanyika Februari tarehe 18 mwakani.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amevitaka vyama vyote vya kisiasa vilivyo na nia ya kushiriki uchaguzi huo kuwasilisha majina ya wagombea wake ifikiapo Desemba tarehe 28, yaani Jumatatu ijayo.
Aidha agombea binafsi wameshauriwa kuwasilisha majina yao kwa IEBC na nembo watakazotumia ifikiapo siku hiyo ya Jumatatu.
Kulingana na IEBC kampeni za uchaguzi huo zitafanyika kati ya Januari tarehe 18 hadi Februari tarehe 15 kati ya saa moja asubuhi na saa kumi na mbili jioni.
Uchaguzi huu mdogo unafuatia kuondolewa kwa aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko kutokana na tuhuma mbalimbali ukiwamo ufisadi.
Ikumbukwe Sonko amewasilisha kesi mahakamani akitaka shughuli ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo isitishwe.
Sonko amesema yu tayari kujitetea mahakamani.
Sonko ameendeela kuwashtumu maseneta kwa kukubali hoja ya kumtimua mamlakani akidai hatua hiyo ilichochewa na misimamo wake mikali dhidi ya serikali.
Tayari wanasiasa mbalimbali wametangaza nia ya kuwania ugavana jijini Nairobi. Miongoni mwao ni aliyekuwa Mbunge wa Starehe Margaret Wanjiru, Peter Kenneth na aliyekuwa Mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru.
Mwingine ni aliyekuwa Gavana wa Kiambu, William Kabogo.
Share this: