
Kamati ya Kiufundi ya Mpango wa Upatanishi, BBI imekusanya saini milioni 1.5 tangu kuanza kwa shughuli hiyo wiki iliyopita.
Ni saini saini milioni moja tu zinazohitaji kufanikisha kufanyika kwa kura ya maamuzi kupitia BBI ila Rais Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga wanakusudia kukusanya saini milioni nne ikiwa njia moja ya kuonesha umaarufu wao sawa na umaarufu wa mchakato wa BBI.
Haya yanajiri huku viongozi mbalimbali wa Ukambani wakiwaongoza wananchi katika kutia saini Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa Mwaka wa 2020.
Shughuli hiyo imeongozwa na Mwakilishi wa Kike wa Makueni Rose Museo katika eneo la Kilome.
Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mwakilishi wadi maalumu Sarah Mulwa amemrai Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake Raila Odinga kutoondoa kiti cha mwakilishi wa kike akisema hilo litaathiri pakubwa uongozi wa jinsia ya kike.
Aliyekuwa Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Kalembe Ndile amemkashifu vikali aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnston Muthama ambaye anaongoza kampeini ya kupinga BBI katika eneo hilo.
Kauli ya Kalembe imesisitizwa na Museo huku akiwataka wakazi wa Ukambani kuunga mkono ripoti ya BBI.