
Kampeni za uchaguzi mdogo katika Eneo la Msambweni kwenye Kwale zikishika kasi, wandani wa Naibu wa Rais, William Ruto wanaendeleza mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali kumpigia debe mgombea huru Feisal Bader.
Wandani hao wakiwamo waliokuwa maseneta Johnstone Muthama na Bony Khalwale wamewataka wakazi kumchagua Feisal kuwa mbunge wao.
Viongozi hao wameandamana na Mbunge wa Lungalunga, Khatib Mwashetani na wamewataka wananchi kuhakikisha wanampigia kura Feisal ili kudumisha heshima ya Gavana wa Kwale, Salim Mvurya ambaye tayari ametangaza kumuunga mkono.
Uchaguzi huo mdogo utafanyika tarehe 15 mwezi ujao huku kivumbi kikitarajiwa kati ya Feisal na Omar Boga wa ODM.
Mapema wiki jana, viongozi wa Chama cha ODM wakiongozwa na Gavana wa Mombasa Ai Hassan Joho walikita kambi katika vijiji kadhaa vya Eneo la Msambweni wakimfanyia kampeni Omar Boga. Seneta wa Kwale Issa Juma Boy akizungumza katika misururu ya mikutano hiyo aliwataka wapinzani wao kuendesha kampeni kwa amani huku Gavana Joho akisisitiza kwamba Boga ndiye chaguo la serikali kwa kuwa Jubilee haikuweka mgombea.
Uchaguzi huo unafanywa kufuatia kifo cha Suleiman Dori.