×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Marekani yawataka raia wake nchini Eritrea kuwa makini kufuatia mapigano nchini Ethiopia

Marekani yawataka raia wake nchini Eritrea kuwa makini kufuatia mapigano nchini Ethiopia

Marekani imesema kwamba kumeshuhudiwa milipuko sita mikali katika mji mkuu wa Eritrea Asmara.

Japo haijataja kilichosababisha milipuko hiyo, inaaminika kwamba imesababishwa na mapigano yanayoendelea nchini Ethiopia.

Ubalozi wa Marekani nchini Eritrea umewashauri raia wake nchini humo kuwa makini  na kufuatilia kwa karibu mapigano hayo.

Ni jana tu ambapo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitangaza kwamba majeshi yake yamechukua mamlaka ya kudhibiti mji mkuu wa Tigray, Mekelle.

Chama cha waasi wa jamii ya Tigray Tigrayan People’s Liberation Front (TPLF), kilisema wanachama wake wanajiondoa katika mji huo.

Mapigano baina ya wanajeshi wa serikali ya Ethiopia na TPLF yaliannza tarehe 4 mwezi huu,  na kusababisha mamia ya watu kufariki dunia na maelfu kuachwa bila makao.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa Linalowashughulikia Wakimbizi UNHCR kusema zaidi ya raia elfu arubaini wa Ethiopia wamehamia taifa jirani la Sudan, huku idadi hiyo ikitarajiwa kufikia elfu mia mbili  katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Mshirikishi wa amani wa UNHCR nchini Ethiopia Mohamed Rafik alisema hali hiyo inahatarisha maisha ya wakimbizi hata zaidi kwani baadhi ya kambi zinawahifadhi watu wengi zaidi kuliko kiwango kinachohitajika kipindi hiki cha korona.