
Shughuli ya kutia saini mswada wa marekebisho ya katiba wa mwaka 2020 miongoni mwa Wakenya imezinduliwa katika maeneo mbalimbali nchini huku viongozi wakiendelea kuupigia debe.
Akizungumza kwenye Kaunti ya Kakamega, Gavana Wycliffe Oparanya amewataka machifu na manaibu wao vilevile maafisa wa utawala kwenye wadi kushirikiana katika kuhakikisha kwamba saini milioni moja zinapatikana katika muda wa wiki moja.
Katika hafla tofauti, viongozi wa kaunti za Kisii na Nyamira wakiongozwa na Gavana James Ongwae na Seneta Sam Ongeri wamesema watahakikisha asilimia themanini ya wakazi wanashiriki shughuli hiyo muhimu.
Kwingineko Kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto amezindua shughuli iyo hiyo katika eneo la Kusini mwa Bonde la Ufa, Ruto akilenga kupata saini elfu mia mbili.
Akizungumza katika kaunti ya Bomet akiandamana na Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu KNUT Wilson Sossion, Ruto amewaomba Wakenya kujitokeza kwa wingi akisema huenda shughuli hiyo ikachukua siku tatu pekee kutokana na idadi kubwa ya watu wanaojitokeza kuunga BBI.
Kwenye Kaunti ya Laikipia Mwakilishi wa Kike wa kaunti hiyo Cate Waruguru ameendeleza kampeni sawa na hizo akiwahimiza Wakazi kuwajitokeza kwa wingi na kusaini mswada huo.
Kwenye Kaunti ya Uasin Gishu shughuli hiyo imezinduliwa na Mwenyekiti wa ODM katika kaunti hiyo Kipkorir Menjo baada ya nakala 320 za ripoti ya BBI kusambazwa.
Hata hivyo, wakazi wa kaunti hiyo wamesema hawatatia saini hadi watakapoisoma ripoti yenywe na kuielewa.