×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

ANC inaunga mkono mswada wa kufanyia katiba marekebisho, Mudavadi

ANC inaunga mkono mswada wa kufanyia katiba marekebisho, Mudavadi

Chama cha ANC, kimetangaza kuunga mkono kikamilifu mswada wa kuifanyia katiba marekebisho kupitia Mpango wa Upatanishi, BBI.

Kinara wa chama hicho Musalia Mudavadi anasema mapendekezo yote yalioibuliwa baada ya uzinduzi wa ripoti ya pili yamejumuishwa.

Akifafanua baadhi ya mapendekezo ambayo yamejumuishwa katika mswada huo mpya, Mudavadi amesema jinsi ilivyo sasa, mswada huo utawanufaisha Wakenya pakubwa hivyo ANC itakuwa katika mstari wa mbele kupigia debe.

Ameipongeza kamati ya BBI kwa kuhakikisha ugatuzi unalindwa, idara ya polisi haiingiliwi kisiasa vilevile seneti kupewa nguvu zaidi.

Akihutubia wanahabari katika makao makuu ya ANC, Mudavadi aidha amepigia upatu pendekezo la kuipa Nairobi hadhi maalumu ili gavana atakayechaguliwa achukue majukumu yote baada ya Idara ya Jiji la Nairobi, NMS kukamilisha muhula wake. Amesema ni kupitia pendekezo hili ambapo ugatuzi utapigwa jeki jijini.

Kuhusu pendekezo la Kiongozi wa Upinzani vilevile Waziri Mkuu, Mudavadi amesema wawili hao hawatateuliwa kutoka katika chama kimoja. Mudavadi anasema mswada huo mpya umeweka bayana kuhusu majukumu ya wawili hao na kwamba kiongozi wa upinzani sharti awe na asilimia 25 ya wajumbe katika bunge.

Pia amesema mswada wa sasa umeweka wazi jinsi maeneo bunge zaidi 70 yatakavyobuniwa tofauti na awali ambapo haikuwekwa wazi. Amesema baada ya uchaguzi mkuu ujao, bunge litakuwa na wajumbe 360. Kiongozi huyo kadhalika amezungumzia suala la uteuzi wa wabunge wanawake ili kuafikia uwakilishi wa kijinsia.

Ufafanuzi huo wa Mudavadi kuhusu masuaja kadhaa unajiri huku Kinara wa ODM, Raila Odinga akijitetea kutokana na madai kwamba huenda hakuwa na ufahamu wa marekebisho yaliyofanyiwa ripoti ya BBI.  Jana Raila alitetea uteuzi wa Makamishna wa IEBC kufanywa na vyama vya kisiasa ilhali pendekezo hilo halipo katika ripoti ya mwisho ya BBI.

Katika taarifa, Msemaji wa Raila, Dennis Onyango amesema Raila ana ufahamu wa mabadiliko yote yaliyofanywa na kwamba alichofanya jana ni kufafanua pendekezo la awali lililozua ubishi vilevile kusisitiza kwamba mapendekezo yote yakiwamo yake yasingejumuishwa.