
Serikali za Kaunti zimesema kwamba licha ya kuimarisha juhudi za kukabili maambukizi ya virusi vya korona, hakuna vituo vya kutosha vya kufanyia vipimo kubaini iwapo mtu ameambukizwa korona au la.
Baraza la Magavana limesema hali hiyo inaathiri pakubwa vita dhidi ya maambukizi hayo ambayo yameendelea kuongezeka miongoni mwa jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Afya wa Baraza la Magavana, ameiambia Kamati ya Seneti ya Afya kwamba Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu KEMRI inastahili kuhakikisha kwamba kaunti zote zina vituo vya kutosha.
Hayo yanajiri huku KEMRI ikiieleza kamati hiyo kwamba ina uwezo wa kufanyia vipimo sampuli elfu kumi kila siku kwenye sehemu mbalimbali nchini.
Akizungumza mbele ya kamati hiyo, Afisa Mkuu Mtendaji wa taasisi hiyo Yeri Kombe amesema kwamba, katika vituo vingi KEMRI ina uwezo wa kuzipima sampuni elfu nne, ila kwa sasa Kituo cha Nairobi na Kisumu ndivyo vinavyoongoza kwa kupima sampuli nyingi kwa siku ambazo ni elfu moja mia tano.
Wakati uo huo, Kombe amesema vituo vyote vya KEMRI vinavyoendesha vipimo vya COVID-19 kote nchini vilifanyiwa ukaguzi na kuidhinishwa kabla ya kuruhusiwa kuanza kuhudumu. Amesema maafisa wote pia wamehitimu.
Hata hivyo ,amesema changamoto kuu ni ukosefu wa wafanyakazi wa kutosha na mashine za kutosha huku akiiomba serikali kuirusu taasisi hiyo kuwaajiri wafanyakazi zaidi.