×
x Digital News Videos Opinions Cartoons Education U-Report E-Paper Lifestyle & Entertainment Nairobian SDE Eve Woman Travelog TV Stations KTN Home KTN News BTV KTN Farmers TV Radio Stations Radio Maisha Spice FM Vybez Radio Enterprise VAS E-Learning Digger Classified The Standard Group Corporate Contact Us Rate Card Vacancies DCX O.M Portal Corporate Email RMS
Login ×

Ukusanyaji wa saini milioni moja kuzinduliwa leo

Ukusanyaji wa saini milioni moja kuzinduliwa leo

Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake Raila Odinga wanatarajiwa leo hii kuzindua rasmi Mswada wa Marekebisho ya Katiba na ukusanyaji wa kitaifa wa saini milioni moja katika Ukumbi wa KICC.

Licha ya kuwa ni saini milioni moja tu zinazohitaji kuifanyia katiba marekebisho kupitia ripoti ya Mpango wa Upatanishi, BBI viongozi hao wanalenga kukusanya saini milioni nne na iwapo watafaulu basi hali hiyo itaonesha kwamba BBI ina umaarufu mkubwa.

Miongoni mwa viongozi ambao wamealikwa kuhudhuria hafla hiyo ni Kinara wa ANC, Musalia Mudavadi, mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula, wa Wiper Kalonzo Musyoka na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU Francis Atwoli.

Tayari Tume ya Uchaguzi, IEBC imeidhinisha fomu itakayotumika kukusanya saini hizo.

Katika barua iliyotumwa kwa Kamati ya BBI, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati amesema fomu hiyo imeidhinishwa kwa kuzingatia sheria.

Kulingana na mpangalio, mpiga kura aliyesajiliwa atahitajika kujaza jina lake, nambari ya kitambulisho ama paspoti, kaunti, eneo bunge, wadi na kisha kutia saini.

Viongozi wa Kamati ya Kitaifa ya BBI Dennis Waweru na Junet Mohamed, wamesema baada ya uzinduzi huo, shughuli hiyo itafanyika katika kaunti zote arubaini na saba.

Shughuli hiyo iliahirishwa wiki iliyopita kutokana na kucheleweshwa kwa mswada wa marekebihso ya katiba ambao umekamilika.

Uzinduzi wa leo utafanyika huku makundi mbalimbali, viongozi wa kidini na wanasiasa hasa wanaoegemea mrengo wa Naibu wa Rais William Ruto wakiendelea kushinikiza baadhi ya vipengele kurekebishwa na mapendekezo yao kujumuishwa.

Ruto, amekuwa akipendekeza mazungumzo kufanyika ili mwafaka kupatikana kuhusu baadhi ya vipengele ambayo vinaibua utata ili kuzuia kuwapo kwa kura ya ushindani.

Hayo yamejiri huku Odinga akisema kwamba marekebisho yaliyopendekezwa yamejumuishwa katika mswada huo .