
Naibu wa Rais William Ruto ameikosoa hatua ya Idara ya Upelelezi DCI kufungua upya faili za kesi za ghasia za baada ya uchaguzi, akisema hatua hiyo huenda ikawagawanya Wakenya hata zaidi.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa twitter, Ruto amesema hatua hiyo inalenga kuibua ukabili na hivyo kulemaza juhudi za kuliunganisha taifa.
Amesema umasikini vilevile ukosefu wa ajira vinasalia kuwa changamoto kuu miongoni mwa wakenya na wala si ukabila.
Awali viongozi wa Eneo la Bonde la Ufa wakiongozwa na Gavana wa Uasin Gishu Jackosn Mandago, Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen vilevile Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi walimkosoa Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi DCI wakisema kuwa hatua yake huenda ikaibua uhasama baina ya Wakenya.
Katika kauli ambayo ilisisitizwa na Seneta wa Nakuru Susan Kihika, viongozi hao walisema kuwa Jamii zilizozozana zilisameheana na kuamua kuishi kwa utangamano bila kujali kabila wala dini na kwamba kufufuliwa kwa kesi hizo kutalirejesha taifa nyuma.