
Shughuli za matibabu zimetatizika kwenye Hospitali za Kaunti ya Elgeyo Marakwet baada ya wahudumu wote wa afya kugoma kulalamikia hatua ya Serikali ya Kaunti hiyo kutotii mkataba wa maelewano, CBA. Ni hali ambayo imewasababishia wakazi mahangaiko huku waliokuwa wamelazwa kwenye hospitali mbalimbali za kaunti hiyo wakilazimika kuondoka na kusaka matibabu kwingine.
Kwa kawaida hospitali hii ambayo ni hospitali kubwa zaidi katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet hufurika watu kutoka maeneo mbalimbali wanaosaka matibabu.
Hali imekuwa tofauti leo baada ya wahudumu wote wa afya kuanza mgomo wakidai kutoangaziwa kwa maslahi yao, hali ambayo imewasababishia wagonjwa mahangiko chungu nzima.
Erick Kwambai mkazi wa eneo la Bugar amelazimika kuwaondoa wanawe wawili waliokuwa wamelazwa hospitalini humu baada ya kupigwa na nguvu za umeme.
Kwa upande wake Alex Kiprono Koech amesalia na machungu baada ya mkewe kuchelewa kufanyiwa upasuaji ili kumsaidia kujifungua na kusababisha mwanao kuaga dunia.
Wahudumu wa afya wa kaunti hii wamekuwa katika mgomo baridi tangu wiki iliyopita wakiishinikiza serikali ya kaunti kuwaongezea mishahara na kuwapandisha vyeo.
Wakiongozwa na Afisa Mshirikishi kati ya Chama cha Madaktari KMPDU na Madaktari wa Kaunti hii, Maurice Chebasa mapema leo waliandamana hadi kwenye ofisi ya Bodi ya Huduma za Umma wakimshtumu mwenyekiti wa bodi hiyo Michael Lelit kwa kutowapa barua waliofaa kupandishwa cheo.
Hata hivyo Lelit amejitetea akisema kuwa wahudumu hao watapata barua haraka iwezekanavyo.