
Huduma katika hospitali za umma nchini huenda zikaathirika hata zaidi kufuatia ilani ya mgomo ya wahudumu mbalimbali wa afya.
Muungano wa Maafisa wa Kliniki, KUCO umetoa makataa ya siku kumi na nne ya mgomo, ukilalamikia hatua ya serikali kuwatekeleza wakati huu wa korona kwani wengi wao hawana vifaa vya kujikinga, PPEs.
Aidha, wamelalamikia kutolipwa marupurupu yao licha ya kutia saini mkataba wa maelewano. Haya yanajiri siku moja tu baada ya afisa mmoja wa kliniki, Dakta Nira Patel kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.
Muungano huo unasema vifo vyote vinavyohusisha wahudumu wa afya vinatokana na kutozingatiwa kwa masharti ya kujilinda dhidi ya virusi hivyo.
Vilevile umelalamikia uongozi wa hospitali mbalimbali kutowapa likizo wahudumu wanaogua magonjwa hatarishi. Peterson Wachira ni Mwenyekiti wa muungano huo.
Haya yanajiri wakati ambapo madaktari chini ya Chama cha KMPDU wakiwa wametangaza mgomo baada ya kukamilika kwa siku 21.
Vilevile madaktari hao wanalalamikia kutolipwa marupurupu, bima ya afya inayoshughulikia magonjwa sugu kama korona miongoni mwa malalamiko mengine.
Ikumbukwe takriban wahudumu wa afya thelathini na wawili wamefariki kutokana na Covid-19.