
Idara ya Upelelezi DCI inaendelea kulichunguza kundi la watu linaowahadaa wasichana wadogo hasa wa shule za upili kuhudhuria sherehe zinazofanyika kwenye maeneo mbalimbali jijini Nairobi na ambazo huendelea kwa siku kadhaa.
DCI ikizungumzia kisa cha jana ambapo wasichana sita waliotoweka nyumbani kwao kisha kuokolewa, imesema kuna kundi la watu linalotumia kipindi hiki cha korona kuwapotosha wanafunzi.
Kupitia mtandao wa Twitter idara hiyo imeonya vikali dhidi ya vitendo hivyo ikisema wanaohusika watakabiliwa vikali kwa mujibu wa sheria.
Wakati uo huo, imewashauri wazazi kuwa makini na wanao, kujua waliko kila wakati na kufahamu wanachofanya hasa kupitia mitandao ya kijamii.
Ikumbukwe msichana mmoja angali anatafuwa huku wenzake wakiwa bado wanahojiwa na maafisa wa DCI wanaosimamia kitengo cha watoto.
Kulingana na taaarifa ya Idara hiyo ni kwamba wasichana hao wamewaelezea jinsi walivyohadaiwa na kundi la Carty-gang-ent kupitia mitandao ya kijamiii, huku ikibainika kwamba linatumia nambari za simu za kimataifa ila liko hapa jijini Nairobi.
Wasichana hao walipatikana baada ya video moja ya mwanamke mmoja kusambaa mitandaoni akisema binamu yake alitoweka na wenzake sita ambao walihadaiwa na Mzungu mmoja kwa simu, kwamba wangewatafitia ajira ya pesa nyingi baada ya kuwahoji.
Share this: